NA HAPPINESS SHAYO
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza amekabidhi mitaji ya biashara, mitungi ya gesi 66, pikipiki moja na kompyuta moja kwa kinamama wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania, Wilaya ya Ukerewe lengo ikiwa ni kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Mhe. Masanja amekabidhi vitu hivyo leo alipotembelea ofisi za Umoja wa Wanawake Tanzania, Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.

“Nimekuja na mtaji wa shilingi laki moja moja kwa kila mwanamke, fedha hizi sasa zikasaidie kuongeza vipato vyenu kwa kufanya biashara ndogondogo,” Mhe. Masanja amefafanua.
Kuhusu mitungi ya gesi ,Mhe. Masanja amesema lengo ni kuwasaidia kinamama hao kutumia nishati mbadala na kuachana na matumizi ya kuni ambazo ni chanzo cha uharibifu wa mazingira.
“Nimekuja na nishati mbadala ambayo itasaidia kinamama hawa kuondokana na changamoto za kutafuta kuni na kwa wakati huo huo watakuwa wanatunza mazingira,”amesema Mhe.Masanja.


Aidha, Mhe. Masanja amesema pikipiki aliyoikabidhi itumike kuongeza mapato ya umoja huo ili waweze kukua kiuchumi na pia kompyuta hiyo itumike katika shughuli za kiofisi za Umoja huo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mary Masanja ameahidi kushirikiana na wanawake hao kumaliza ujenzi wa jingo la UWT Ukerewe.
Awali akizungumzia kuhusu utalii wa utamaduni, Mhe. Mary Masanja amesema Serikali inaunga mkono jitihada za watanzania wanaojihusisha na ngoma za asili na hivyo itahakikisha inainua vipaji vya watanzania hao.


Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Ukerewe, Neema Mgobela amemshukuru Mhe. Mary Masanja kwa msaada huo.
“UWT Ukerewe unakushukuru sana kwa upendo uliouonyesha siku ya leo na umedhihirisha kwamba sana viatu tulivyokuvisha vimekutosha na uendelee kupambana,”amesema.



Ameahidi kinamam hao wataenda kutumia vyema mitaji hiyo kuzalisha vipato vyao ili kukua kiuchumi.
“Kinamama wa Wilaya hii wanakuahidi kumiliki uchumi kwa sababu umetupa kianzio na sisi tutaenda kufanya shughuli zetu za ujasiriamali ili kuunga jitihada zako ulizotuonyesha leo,”amesema Bi. Mgobela.