NA MWANDISHI MAALUM
NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga (Mb) ameipongeza Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa maendeleo mazuri ya mradi wa ujenzi wa Ofisi na Maabara ya Kanda inayoendelea kujengwa jijini Mwanza.
Mhe. Naibu Waziri ameyasema hayo leo jijini Mwanza alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Maabara ya TAEC eneo la Nyegezi ambapo amewaambia wananchi kuwa jukumu la Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi hivyo kupitia Maabara hiyo udhibiti wa matumizi salama ya Mionzi utafanyika kwa ufanisi na hivyo kuwalinda wananchi wa Kanda ya Ziwa juu ya madhara yanayoweza kusababishwa na Mionzi.
Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Prof. Lazaro Busagala ameishukuru serikali kwa kuendelea kuelekeza nguvu na kutenga fedha kwa ajiri ya miradi mbalimbali inayosogeza huduma kwa wananchi huku akisema kuwa kwa sasa wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa sasa vibali vya mionzi vinatolewa ndani ya muda mchache na kwa muda usiozidi siku moja kibali kinapatikana tofauti na ilivyokuwa awali ambapo ilikuwa ikichukua hadi muda wa siku saba ili mteja kupata kibali.
Maabara hii ya kanda inajengwa na Serikali kwa kiasi cha shilingi Bilioni 2.8 ambapo jumla ya mikoa nane (8) ya Kanda ya Ziwa itakuwa ikipata huduma kupitia Maabara hii.
Ni juhudi nyingine ya Serikali katika kufikisha huduma kwa wananchi na kuwawezesha wafanyabiashara kupata vibali vya Mionzi kwa wakati hivyo kuharakisha na kuwezesha Biashara.
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ni Taasisi ya Serikali iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Namba 7 ya Mwaka 2003 ikifuta Sheria ya Bunge Namba 5 ya Mwaka 1983 iliyokuwa imeunda Tume ya Taifa ya Mionzi
Majukukumu ya TAEC ni; (i) Kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini, (ii) Kuhamasisha na kuendeleza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na (iii), kufanya tafiti na kutoa taarifa mbalimbali juu ya sayansi ya teknolojia ya nyuklia.