Nyasho FC yatwaa Kombe la Mbunge (Mathayo Cup) kwa kuichapa Makoko FC 4-2

NA FRESHA KINASA

TIMU ya Nyasho FC iliyopo Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara imeibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Makoko FC katika mchezo mkali na wakusisimua wa fainali ya Kombe la 'Mathayo Cup'.

Ni mchezo uliochezwa katika dimba la kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma na kufanikiwa kutwaa taji hilo kwa mwaka 2020/2021 pamoja na zawadi ya ng'ombe mwenye thamani ya Shilingi Milioni 2 huku timu ya Makoko FC ikipata zawadi ya Shilingi 300,000 kwa kuwa mshindi wa pili na Bweri FC mshindi wa tatu Shilingi 200,000.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt.Halfan Haule akimkabidhi kikombe nahodha wa timu ya Nyasho FC baada ya kuichapa Makoko FC mabao4-2 katika Fainali ya 'Mathayo Cup' .
Timu ya Nyasho FC ilipata bao la kwanza kipindi cha pili likifungwa na Iddi Shabani dakika ya 48, na goli la pili lilifungwa na Joshua Marlaw dakika ya 67 na goli la tatu lilifungwa dakika ya 72 na Iddi Shabani huku bao la 4 likifungwa na Dionizi Ndalu dakika ya 80 na mabao ya Makoko yakifungwa na Julius Joseph dakika ya 53 na Zedekia Donald dakika ya 90 ya mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wengi kutoka viunga vya Musoma.

Mchezo huo wa fainali umechezwa leo Desemba 9, 2021 katika kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika na kutanguliwa na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa netibali, burudani ya mziki, kula mkate na kunywa soda kwa dakika tatu, mbio za miguu pamoja na mchezo wa kusaka nafasi ya tatu iliyochukuliwa na timu ya Mwigobero baada ya kuichapa timu ya Kitaji mabao 4-3 kwa njia ya mikwaju ya penati kufuatia dakika 90 kumalizika bila kufungana.
Michuano ya kombe la "Mathayo Cup" iliandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mheshimiwa Vedastus Mathayo na kushirikisha timu 16 za Manispaa ya Musoma ambapo pia wachezaji bora waliopatikana baada ya michuano hiyo watasimamiwa na kuendelezwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini ili kukuza vipaji vyao.

Akikabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali Mkuu wa Wilaya ya Musoma,Dkt. Halfan Haule amewataka vijana kuwa waadilifu na kuhakikisha wanajenga utaratibu wa kufanya mazoezi ili kujimarisha kiafya sambamba na kujenga uhusiano mwema katika jamii.

Amesema, vijana ni nguvu kazi ya taifa hivyo wanawajibu wa kuonesha uwajibikaji kwa shughuli za maendeleo na kutumia fursa mbalimbali zinazowazunguka katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Mathias Peter ni mkazi wa Kata ya Kitaji ambapo amempongeza Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo kuanzisha michuano hiyo kwani imeleta hamasa na uhusiano mwema baina ya vijana wa kata za Manispaa ya Musoma.

Juliana Shabani Mkazi wa Kata ya Bweri amesema, Mbunge Mathayo amekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha vijana kupitia fursa mbalimbali na hivyo kuwafanya wawe pamoja na kusaidia kupunguza vitendo vya kihalifu ndani ya jamii.
Katika hatua nyingine upande wa michezo ya netbali imechezwa kati ya Bweri na Mwisenge ambapo Bweri imeibuka kidedea kwa kupata mabao 13, na Mwisenge mabao 12, huku mshindi wa tatu ikichukuliwa na Rwamulimi baada ya kuichapa timu ya netiboli ya Nyasho mabao 22-10.

Washindi wa michezo mbalimbali wamekabidhiwa zawadi na vyeti vya ushiriki na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt.Halfan Haule aliyekuwa mgeni rasmi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news