NA MWANDISHI MAALUM
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe ametoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Waziri wa OR-TAMISEMI, Ummy Mwalimu kupiga marufuku utaratibu wa Shule za Msingi na Sekondari kuwazuia wanafunzi kwenda likizo na kusoma hadi usiku katika muda wa ziada.
Profesa Shemdoe amesema, kupitia Marekebisho ya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978,zilitungwa kanuni za Elimu za mwaka 2002.
Amesema, sheria na kanuni hizo zinaweka idadi ya siku za masomo kwa mwanafunzi katika mwaka wa masomo husika, kuwa ni siku 194 kwa shule za msingi na sekondari ukiondoa Jumamosi na Jumapili, sikukuu za umma na likizo.
Profesa Shemdoe amesema, maagizo hayo ya yanapaswa kusimamiwa kikamilifu na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo ndiyo yenye jukumu la kutekeleza maelekezo ya Kisera na Kisheria.
"Kanuni hizo hazikuacha ombwe katika usimamizi, zimeeleza endapo siku za masomo zitapotea kwa sababu zilizo nje ya udhibiti wa shule au Mamlaka shule au Mamlaka hiyo itapaswa kuomba kibali cha kufidia siku Hizo kwa kamishna wa elimu na katika kibali chake kamishna ataeleza muda wa kusoma wakati wa likizo. Hiyo ni kwa shule zote za Serikali au Binafsi,"amesema.
Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Prof. Shemdoe amesema, Wizara imefanya hivyo kwa kutambua Likizo ni Muda wa mtoto kupumzika na hivyo kuwa na uwezo wa kufatilia masomo vizuri katika muhula unaofuata.
Amesema, muda wa likizo humwezesha mtoto kuwatembelea na kuchangamana na ndugu, jamaa, na marafiki na hivyo kukuza stadi zisizokuwa za kitaaluma.
"Watoto wetu ni zao la jamii tusijaribu kuitenga elimu na jamii, pia tuwape watoto wetu fursa ya kujifunza shughuli ndogo ndogo za kijamii na kiuchumi kama vile usafi wa mazingira, kilimo, upishi, ujenzi na ujasiriamali" Prof. Shemdoe.
Katibu Mkuu amezitaka shule zote za Serikali na Binafsi kuhakikisha zinazingatia sheria hiyo.