NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ina azma ya kukiimarisha Kikosi cha Zimamoto ili kukabiliana na athri kubwa zinazotokana na matukio ya moto katika hoteli za kitalii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) alipotambulishwa na kuwasalimia viongozi katika Hoteli ya Tui Bluu Bahari Zanzibar na Mkurugenzi Mtendaji Reda Sweed (kushoto) iliyopo Kijiji cha Pwanimchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja Desemba 11,2021 alipofika rasmi kwa ajili ya kuifungua. (Picha zote na Ikulu).
Dkt.Mwinyi amesema hayo katika hafla ya uzinduzi mpya wa Hoteli ya Kitalii ya Tui Blue Bahari Zanzibar huko Pwanimchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya hoteli hiyo iliyoungua Januari 16, 2021 kufanyiwa ukarabati mkubwa na kuanza kutoa huduma.
Amesema, kumekuwa na matukio mengi ya moto ya kuungua moto hoteli za kitalii, hivyo Serikali inajipanga kukiimarisha Kikosi cha Zimamoto ili kukabiliana na hali hiyo ambayo imekuwa ikileta athari kubwa katika sekta ya Utalii
Amesema, Serikali ina kila sababu ya kuunga mkono sekta ya Utalii kwa kuzingatia kuwa hiyo ndio sekta mama ya kiuchumi.
Alieleza kuwa, uweekezaji katika Sekta ya Utalii una mambo matatu yanayolinufaisha Taifa ikiwemo ajira, wananchi kupata soko la kuuzia bidhaa zao pamoja na Serikali kupata fedha zitokanazo na kodi, na hivyo akabainisha azma ya Serikali ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na viongozi wa Vikosi vya Ulinzi kwa kupokea saluti ya heshima mara alipofika katika Hoteli ya Tui Bluu Bahari Zanzibar iliyopo Kijiji cha Pwanimchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofika rasmi kwa ajili ya kuifungua.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Tui Bluu Bahari Zanzibar Bw.Reda Sweed (kushoto) pamoja na Mkuu wa wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Mhe.Ayoub Mohamed Mahamoud (kulia) na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe.Lela Mohamed Mussa (wa pili kulia) alipotembelea sehemu mbalimbali na kuangalia vyumba katika Hoteli Tui , mara baada ya kuifungua rasmi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuimarisha sekta hiyo ili kuvutia watalii, na ndio maana ikaingia mkataba na Kampuni ya ADNATA kutoka Dubai ili kuimarisha shughuli utoaji wa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume pamoja na kuunda kikosi cha Utalii ili kuwahakikisha watalii usalama wao wakati wanapofika nchini.
Amesema, wawekezaji katika Sekta ya Utalii wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi, ikiwemo afya, elimu na maji na hivyo akazitaka mamlaka zinazohusiana na utalii kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha wananchi wa maenoe ya uwekezaji wananufaika ipasavyo.
Nae, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohamed Mussa alisema kurejea kwa huduma katika hoteli hiyo kunatokana na juhudi za mwekezaji wake kujitoa na kufanya kazi usiku na mchana na hatimae kufanikiwa kurejesha huduma hizo ndani ya kipindi kifupi na kwa kiwango bora zaidi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi (katikati) akikata utepe kama ishara ya Ufunguzi wa Hoteli ya Tui Bluu Bahari Zanzibar iliyopo Kijiji cha Pwanimchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofika rasmi kwa ajili ya kuifungua, akiwepo Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe.Lela Mohamed Mussa (wa tatu kulia) pamoja na Viongozi wa Hoteli waliohudhuria hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA),Shariff Shariff (kushoto) akiwa pamoja na Wasaidizi wa Rais katika hafla ya Ufunguzi wa Hoteli ya Tui Bluu Bahari Zanzibar iliyofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika Kijiji cha Pwanimchangani Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema, kurejea kwa huduma hizo kutaimarisha sekta ya utalii kwa kutoa ajira kwa vijana, sambamba na kuchangia kikamilifu pato la Taifa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Ayoub Moahmed Mahamoud alisema miongoni mwa mafanikio ya mkoa huo katika kukuza uwekezaji, ni pamoja na kumaliza migogoro mbalimbali, ikiwemo ule wa Hoteli ya Palolo na kubainisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Mkoa na Wawekezaji umekuwa chachu ya mafanikio hayo.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sharif Ali Sharif alisema ufunguzi wa hoteli hiyo umekuja kutokana na hoteli hiyo kufanyiwa matengenezo makubwa baada ya ajali ya kuungua moto na kusababisha uharibifu mkubwa wa samani na baadhi ya majengo.
Amesema, ZIPA inaendelea kutoa pole kwa wamiliki wa hoteli hiyo, sambamba na kutoa pongezi kwa uongozi kutokana na juhudi kubwa za kufanikisha kuifanyia matengenezo hoteli hiyo kwa zaidi ya vyumba 100.
Baadhi ya viongozi na wananchi walioalikwa katika Ufunguzi wa Hoteli ya Tui Bluu Bahari Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) alipokuwa akitoa hutuba yake katika hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Pwanimchangani Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akipokea zawadi maalum kutoka kwa Uongozi wa Hoteli ya Tui Bluu bahari Zanzibar katika hafla ya Ufunguzi wa Hoteli hiyo katika Kijiji cha Pwanimchangani Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema, kiasi cha Dola za Kimarekani 700,000 zimetumika kwa ajili ya uwekaji wa vifaa vya kisasa vya usalama wa hoteli ili kujikinga na majanga.
Aidha, Meneja wa Hoteli hiyo Eric Freinut aliipongeza Wizara ya Mambo ya Kale na Utalii kwa kuuunga mkono kikamilifu juhudi za kuifanyia matengenzo makubwa hoteli hiyo hadi kurejea katika hali yake ya kawaida.
Hoteli ya Tui Blue Bahari Zanzibar, ni hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na Kampuni ya Zanzibar Beach Village iliyoanza na uwekezaji mwaka 2007 , ambapo uwekezaji huo ulianza na mtaji na Dola za Kimarekani zipatazo Milioni 17 na kuongezeka hadi kufikia Dola Milioni 47 kabla ya ajali ya kuungua moto.Hoteli hiyo imeajiri wafanyakazi 258 kati ya hao ni 17 pekee ndio wageni.