NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakubaliana na hatua zilizoanza kuchukuliwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika kuufanyia masahihisho muundo wa utumishi ili kuhakikisha wahadhiri na wafanyakazi wa chuo hicho wanalipwa kwa mujibu wa nafasi zao, muda na kiwango cha elimu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwatunuku Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, watika wa hafla ya mahafali ya 17 ya chuo hicho yaliofanyika katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.(Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi ambaye pia ni Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), amesema hayo katika Mahafali
ya 17 ya chuo hicho, yaliofanyika katika Ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed
Shein, uliopo Tunguu Mkoa Kusini Unguja.
Amesema, kwa
kutambua juhudi zinazofanywa na wahadhiri na wafanyakazi wa chuo hicho,
Serikali inakubaliana na hatua zilizoanza kuchukuliwa na Uongozi wa chuo hicho katika kuangalia upya na kuufanyia masahihisho muundo wa utumishi ili kuhakikisha kila mmoja anapata stahiki zake kwa mujibu wa
nafasi, muda wa utumishi na kiwango cha elimu.
Alieleza kuwa ,
Serikali inatambua kuwepo kwa taratibu za upandaji wa madaraja kwa
taasisi za elimu nchini, hivyo akabainisha suala hilo kuzingatiwa
kikamilifu.
Aidha, alisema Serikali ina azma ya kushirikiana na uongozi wa chuo hicho pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
katika kuitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa wahadhiri na
watumishi wengine wa chuo hicho, ili kuziba nafasi zilizo wazi kufuatia
hatua ya Serikali ya kuwateua wahitimu wengi kushika nafasi mbalimbali
za uongozi Serikalini. Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wakati wa hafla ya Mahafali ya 17 ya Chuo hicho yaliofanyika katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.(Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi
aliutaka uongozi wa SUZA kuandaa utaratibu mzuri wa kupata wahadhiri
miongoni mwa waihitimu wake bora, sambamba na kuwaendeleza wahitimu
waliopo na watumishi wa kada nyingine, kwa kuandaa program maalum za
mafunzo ili kupanua wigo na kuwawezesha wale wenye sifa na ambao bado
hawajapata mafunzo; kupata nafasi hizo.
Amesema , uongozi wa chuo hicho una wajibu wa kutafuta njia mbadala za kupata
fedha ikiwemo mikopo na kuanzisha miradi ya maendeleo iyakayokiletea
faida chuo hicho, na akibainisha kuwa mfumo wa aina hiyo umekuwa
ukitumiwa na vyuo mbalimbali duniani kama njia ya kuharakisha ujenzi wa
miundombinu ya aina mbalimbali ya chuo.
“Nikupeni
moyo kuwa Serikali ipo tayari kutoa dhamana , kwa taasisi za fedha kwa
mikopo ambayo tutajiridhisha itakisaidia chuo kufanikisha utekelezaji
wa miradi ya maendeleo,”amesema.
Alieleleza kuwa, chuo kikuu ni taasisi na kiungo cha ushirikiano kati yake na watu, hivyo
akatoa wito wa kuwa na mashirikiano na vyuo vikuu vingine ili
kujifunza mambo mapya, kubadilishana uzoefu, kushirkiana katika masuala mbalimbali ya kitaaluma pamoja na kufanya tafiti.
Katika
hatua nyingine, Dkt.Mwinyi aliwapongeza wahitimu wote, hususan wa kike
kwa kuwa na idadi kubwa ya wahitimu, ikilinganishwa na wanaume pamoja na
kushika nafasi nyingi za juu katika masomo mbalimbali.
Amewataka
wahitimu wote kutotosheka na ngazi ya elimu waliyofikia na badala yake
kuanza juhudi za kujiendeleza zaidi kimasomo pamoja na kuwataka
kuitumia vyema taaluma waliyopata katika kujiletea mabadiliko na
kujiajiri au kuajiriwa kwa kuzingatia sifa na uwezo walionao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliofanyika katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.(Picha na Ikulu).
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohammed Said amesema, wizara hiyo ina azma ya kujenga ukaribu na Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) ili kuwawezesha vijana wanaohitimu kuweza kuingia katika
soko la Ajira katika maeneo tofauti Duniani.
Mapema,
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Khamis akiwa pia
ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA),
akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, alisema
katika mwaka wa masomo 2020/2021 Baraza limeweza kusimamia uendeshaji,
wajibu na haki za wahadhiri na wafanyakazi wa chuo hicho, ikiwemo suala
la upatikanaji wa stahiki zao pamoja na upandishaji wa madaraja.
Alieleza
kuwa, baraza hilo lilipata fursa ya kujadili na kuchambua changamoto
mbalimbali zinazowahusu wahadhiri na wafanyakazi wa chuo ili
kuhakikisha ufanisi wa kitaaluma unapatikana, ikiwemo suala la
kupishana sana kwa mishahara.
Aidha, Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Mohamed Makame Haji
alisema mafanikio ya chuo hicho ya kuendelea kutoa idadi kubwa ya
wahitimu kuwa sio jambo la kubahatisha, bali linatokana na juhudi kubwa
zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya elimu nchini.
Amesema, mafanikio hayo
yanatokana na umoja na mashirikiano ya wadau wote wa elimu, ikihusisha
Uongozi wa SUZA pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Baadhi ya viongozi wa Serikali na wageni waalikwa wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika hafla ya Mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu cha SUZA yaliofanyika katika ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.(Picha na Ikulu).
Alieleza
kuwa, katika mwaka huo wa masomo (2020/2021) chuo hicho kilikabiliwa na
changamoto mbali mbali, ikiwemo ya kutokuwa na Dakhalia za kutosha
katika baadhi ya Skuli zake pamoja na kutokuwa na miundombinu bora
katika baadhi ya Dakhalia.
Vile vile alisema
kumekuwepo mrundikano mkubwa wa wahadhiri katika baadhi ya Skuli na
taasisi za Chuo hicho, ikiwemo Chuo cha uongozi wa Fedha Chwaka.
Katika mahafali hayo, jumla ya Wahitimu 1894 wa fani na ngazi mbali
walitunukiwa Vyeti, Stashahada, Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na
Shahada za Uzamivu kutoka taasisi na Skuli mbalimbali za chuo hicho,
ikiwemo Skuli ya Kilimo, Skuli ya Kompyuta,Mawasiliano na Taaluma ya
Habari,Skuli ya Biashara na Taasisi ya Utalii.
Nyingine
ni Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Skuli ya Elimu, Skuli ya Sayansi
Asili na Sayansi Jamii na Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni.
Aidha, katika hafla hiyo Rais Dkt.Mwinyi alitunuku zawadi kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri zaidi katika masomo mbalimbali.