NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali anayoiongoza ina lengo la kuhakikisha inajenga uchumi imara utakaoleta maendeleo kwa wananchi wote.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba Mosi,2021 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar,waliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mjumbe wa Baraza la Wazee wa CCM, Bw.Khatib Ramadhan Iddi, baada ya kumalizika kwa mazungumzo na Ujumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Ofisi Kuu Kisiwandui Zanzibar yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Desemba Mosi, 2021. (Picha na Ikulu).
Katika maelezo yake, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba siasa ni uchumi na siasa ikiwa nzuri na uchumi nao huimarika, hivyo juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha kunajengwa uchumi ulio imara na madhubuti.
Aidha, Rais Dkt.Miwnyi amewaeleza wazee hao mipango na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta za maendeleo ili kuhakikisha uchumi unazidi kuimarika pamoja na vijana kupata ajira na Serikali nayo kupata mapato.
Amesema kuwa, jambo kubwa na la msingi katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kupata maendeleo na kuujenga uchumi wake kuwa imara ni kuwepo kwa amani na utulivu, juhudi ambazo zimechukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanyika.
Rais Dkt.Mwinyi ametumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, kwa kuendeleza utamaduni wao wa kukutanana na kiongozi aliyepo madarakani kwa azma ile ile ya kuzungumza na kubadilishana mawazo.
Ametoa shukurani kwa dua wanazozifanya wazee hao mara kwa mara kwa viongozi wao na kwa nchi yao na kuwasisitiza haja ya kuendelezwa kwa utaratibu huo.
Dkt.Mwinyi pia, aliwaeleza wazee hao juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza za kuhakikisha jengo la kihistoria la Beit al Jaib linajengwa upya na kurudi katika hadhi yake ya asili ujenzi ambao unatarajiwa kuanza rasmi hapo Febuari mwakani.
Pia, Rais alieleza hatua za Serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma za Bima ya Afya ili iwe rahisi kupatikana kwa huduma za afya.
Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza haja na umuhimu wa kuijenga upya nyumba ya Kijangwani iliyokuwa Ofisi ya ASP ambayo kwa sasa imebomoka kwa azma ya kuhakikisha historia haipotei.
Mapema akisoma Tamko la Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Mzee Haji Machano alitoa pongezi kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 pamoja na ushiriki kabambe wa kampeni alizozifanya za uchaguzi huo.
Baraza hilo lilieleza kufarajika na kazi aliyoanza kuifanya wakati alipoingia madarakani kwani uongozi wake wameifurahia ikiwa ni pamoja na kuzunguka katika wilaya zote za Unguja na Pemba na kukagua maendeleo pamoja na kukutana na wananchi ambao walipata fursa ya kueleza matatizo wanayoyakabili.
Pamoja na hayo, Baraza hilo lilimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua katika kuiongoza Zanzibar na kuiweka katika hali ya usalama, amani na utulivu.
“Umekemea rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, umerekebisha mfumo mzima wa elimu na kukarabati utawala, umekemea ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, umechukizwa sana na uingizaji na utumiaji dawa za kulevya nchini na umeunda chombo cha udhibiti na ufuatiliaji, umepanua uchumi wa buluu na kuiweka wizara maalum ya shughuli hizo, umewaita wawekezaji,”imeeleza sehemu ya tamko hilo.
Aidha, baraza hilo lilitoa ushauri kwa Rais Dkt.Mwinyi ikiwa ni pamoja na kushauri kwa kujengwa nyumba ya ASP, iliyopo Kijangwani ambayo ina historia kubwa pia, walishauri kujengwa kwa jengo la Bait el Jaib, kuongeza kasi ya kupiga vita vitendo vya ukatili, ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, uingizwaji wa dawa za kulevya pamoja na kupambana na maradhi ya milipuko.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Wawekezaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero wakiongozwa na Balozi Ami Ramadhan Mpungwe ambapo ambao wapo hapa Zanzibar kwa ajili ya mkutano wa Kampuni hiyo wenye lengo la kupanua shughuli na uzalishaji wa kampuni hiyo ambapo Rais Dkt.Mwinyi aliwapongeza kwa kuamua kufanya mkutano huo hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiongozana na mgeni wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Sukari Kilombero, Balozi Ami Mpungwe, baada ya kumaliza mazungumzo na Ujumbe wake wa wawekezaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero, yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar Desemba Mosi, 2021. (Picha na Ikulu).
Rais Dkt.Mwinyi aliwaeleza waekezaji wa wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombera Dira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uchumi wake ambapo imelenga katika Uchumi wa Buluu na kueleza fursa zilizopo katika uchumi huo huku akiwakaribisha wawekezaji hao kuja kuekeza sambamba na kuwa Mabalozi wa kuitangaza Zanzibar kiuwekezaji.