NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane imechukua juhudi za makusudi za kuimarisha Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Wawekezaji kutoka Nchini China wakifuatilia hutuba ya ufunguzi wa Kongamano la Wawekezaji Kiuchumi kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (iliyokuwa Tanganyika) wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar. (Picha zote na Ikulu).
Dkt. Mwinyi amesema hayo wakati alipofungua Kongamano la Uwekezaji na Maonesho ya Bidhaa za Viwanda kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport – Zanzibar.
Amesema,utendaji wa ZIPA umeimarika baada ya kuanzishwa kituo kimoja kinachotoa huduma za Uwekezaji (one stop centre), kikihusika na utoaji wa vibali vya ukaazi, ujenzi, usajili wa kampuni, masuala ya Kodi pamoja na mazingira.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na baadhi ya Mawaziri wa SMZ na SMT,alipowasili katika viwanja vya Hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaki Zanzibar, kuhudhuria Kongamano la Kiuchumi la Wawekezaji, kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (iliyokuwa Tanganyika).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Uwekazeji Kiuchumi Tanzania ikiwa ni kuelekea katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (iliyokuwa Tanganyika) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, kuwashirikisha Wawekezaji kutoka Nje ya Nchi na Tanzania.
Pia amesema hivi sasa Mwekezaji anaweza kupata kibali cha Uwekezaji ndani ya siku tatu endapo atakamilisha vyema taratibu kabla kwenda kituoni, huku akibainisha malengo ya Serikali ya Mwekezaji kukamilisha usajili huo ndani ya siku moja.
Alieleza kuwa Serikali inakamilisha zoezi la kuwa na Benki ya Ardhi, ikiwa ni hatua ya kutatua tatizo la upatikanaji wa rasilimali hiyo na kubainisha mipango ya kuwepo maeneo ya ardhi yaliotengwa kwa shughuli za uwekezaji.
Aidha, alisema Serikali imetangaza fursa za Uwekezaji katika visiwa vidogo vidogo kumi vilivyopo Zanzibar, huku zoezi la kuwapata wawekezaji likiendelea.
Baadhi ya Mwaziri na viongozi wengine wakiwa katika Kongamano la Uwekezaji kuelekea kilele cha Maaadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika lililofanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaki nje ya Jiji la Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuendelea kuwahamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza miradi yao katika sekta mbali mbali, ikiwemo Afya, Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, nishati na miundombinu huku akibainisha uwepo wa fursa kama hizo katika Uvuvi wa Bahari kuu, Viwanda na ujenzi wa nyumba za makaazi pamoja na Biashara.
Akigusia azma ya Serikali kufanikisha utekelezaji wa Uchumi wa Buluu, Dkt. Mwinyi alisema Serikali inakaribisha Wawekezaji katika utekelezaji wa miradi mbali mbali, ikiwemo Ujenzi wa Bandari kubwa ya kisasa ya Mangapwani inayojumuisha Bandari ya Makontena, Bandari ya mafuta na Gesi, Bandari ya nafaka pamoja na Chelezo kwa ajili ya matengenezo ya Meli.
Aidha, alitilia mkazo uwekezaji katika kuendeleza Uchumi wa Bahari na kutoa wito kwa Wawekezaji kuwekeza miradi yao kwenye sekta ya Utalii ambayo ina fursa nyingi.
“Lengo letu ni kuvutia Wawekezaji wengi zaidi katika ujenzi wa Hoteli za kisasa na vivutio maalum vya Mikutano ya Kimataifa, tayari yapo maeneo maalum tuliotenga na tunayoendelea kuyatangaza kwa Wawekezaji,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi. Sambamba na hilo, alitoa wito kwa Wawekezaji kuwekeza kwenye Uvuvi, hususan uvuvi wa Bahari kuu, akibainisha kuwa bado Bahari haijatumika ipasavyo kutokana na uwekezaji mdogo uliofanyika.
Rais Dkt. Mwinyi alisema katika safari ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kumekuwepo na changamaoto na mafanikio makubwa yaliopatikana katika utekelezaji wa mipango ya kujenga uchumi, ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Alisema, kuanzishwa kwa sheria mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kufanyika kwa maboresho ya baadhi ya sheria kumelenga kuhamasisha na kulinda Uwekezaji, sambamba na kuvutia Wawekezaji.
Washiriki wa Kongamano la Kiuchumi la Wawekezaji wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) wakati akilifungua Kongamano hilo la kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (iliyokuwa Tanganyika) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaji Zanzibar.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza waandaaji wa Kongamano hilo kwa kazi kubwa na nzuri pamoja na Wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi walioshiriki, ikiwemo makundi kutoka China na Misri.
Mapema, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekti wa Baraza la Mapinduzi Awamu ya Sita, Abeid Amani Karume aliwapongeza viongozi wa Serikali zote mbili kwa kuandaa Kongamano hilo lililowajumuisha Wawekezaji na wadau mbalimbali na kuendeleza juhudi za kuliletea Taifa maendeleo katika nyanja tofauti ikiwemo kuimarisha uchumi kwa maslahi ya wananchi wake.
Alisema, juhudi za kuvutia Wawekezaji zitaimarisha uchumi pamoja na kutoa ajira kwa vijana, hivyo akapongeza hatua ya Serikali kuja na Kongamano hilo na kuwashirikisha wananchi wenyewe.
Nae, Waziri wa Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alisema kumekuwepo hatua kubwa zilizochukuliwa katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji, ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa kitovu cha uwekezaji, kuambatana na Sera na Sheria ziliopo.
Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia masuala ya Uwekezaji Geoffrey Mwambe alisema Serikali inahitaji shughuli nyingi za Uwekezaji ili kuweza kutoa fursa pana za upatikanaji wa ajira kwa vijana wa Tanzania sambamba na kuwa na walipa kodi wengi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Cheti cha Pongezi cha Ushindi wa Mlipa Kodi Bora kilichotolewa na TRA Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB,Bi.Ruth Zaipuna,wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Wawekezaji Kiuchumi kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (iliyokuwa Tanganyika) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.
Alisema,kuwepo kwa rasilimali nyingi hapa nchini kunaifanya Tanzania kutokuwa na sababu ya kuwa nyuma kiuchumi, akibainisha faraja iliopo kutokana na Mabenki mbali mbali yaliopo nchini kutumia kikamilifu fursa ziliopo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi,Dkt. Khalid Salum Mohamed alisema kongamanop hilo linatoa fursa kwa Wawekezaji na wadau kutambua fursa za uwekezaji ziliopo katikan Serikali zote mbili za Muungano.
Alitumia fursa hiyo kuwashukuru Wawekezaji na wageni wote walioshirki katika Kongamano hilo muhimu kwa mustakabali mwema wa Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Cheti cha Pongezi kwa kuajiri Wafanyakazi wengi Kagera Sugar Company, Mkurugenzi Mtendaji, S.A.Seif,wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Wawekezaji Kiuchumi kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara (iliyokuwa Tanganyika) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.(Picha zote na Ikulu).
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Sekta binafsi Tanzania (Tanzania Private Setor Foundation – TPSF), Francis Nanai, akigusia mchangao wa sekta binafsi, alisema hivi karibuni Tanzania imeridhia mkataba wa Soko Huru Afrika, na hivyo akabainisha kazi inayoendelea kufanywa na TPSF ya kuwaelimisha Watanzania juu ya jambo hilo, kwa msingi kuwa itawanufaisha wananchi wote.
Alitoa wito na kuwataka kuwa tayari kwa ushindani, sambamba na kufanya ubia na Wawekezaji mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Aidha, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar Hamad Hamad, alisema kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kumeutia nguvu Muungano pamoja na kukuza uchumi na hivyo akabinisha matumaini yake ya kumalizika kwa vikwazo vilivyosalia ambavyo vinasababishwa na watendaji.
Alisema Mamlaka zinazosimamia sekta ya Utalii zina wajibu wa kuwasogeza karibu wadau wa Utalii, kwa lengo la kukuza utalii wa ndani.
Katika Kongamano hilo lilowashirikisha Mabalozi, Mawaziri, Wawekezaji na wageni mbali mbali, Dk. Mwinyi alitoa utambulisho kwa Wawekezaji walipaji wakubwa wa kodi pamoja na waliotoa ajira nyingi.