NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Desemba 11,2021 amekutana na kufanya mazungumzo na wahariri wakiwemo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi amefafanua mambo mbalimbali ambayo yametoa mwelekeo chanya wa Serikali ya Awamu ya Nane anayoiongoza.
Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kuyatolea ufafanuzi baadhi ya masuala aliyoyaeleza katika mkutano wa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake, uliofanyika Hoteli ya Golden Tulip jijini Zanzibar mwezi Novemba 6, mwaka huu.
Uwanja wa Ndege
Katika majadiliano hayo miongoni mwa maswali yalioulizwa na kutolewa ufafanuzi wake ni pamoja na hoja ya Kampuni ya ADNATA kuendesha shughuli za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume jijini Zanzibar.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali imeamua kutafuta kampuni kubwa zenye sifa duniani kushiriki uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Amani Abeid Karume kwa lengo la kutoa huduma bora za kiwango cha kimataifa.
"Huduma bora katika uwanja wa ndege ni moja ya sifa kuu katika kuwezesha soko la utalii kukuwa nchini, ndiyo maana tumefikia hatua hii kwa kutafuta kampuni kubwa ili iweze kuboresha huduma. ADNATA ni kampuni kubwa sana Duniani na inasifika kwa kutoa huduma bora katika viwanja vya ndege katika mataifa zaidi ya 20 Duniani,na uwekezaji wao una maslahi mapana kwa Taifa, badala ya asilimia tano ambazo Serikali ilikuwa inapata kwa shughuli watakazozifanya, Serikali itapata asilimia 12, hii ni hatua njema kwetu,"amesema.
Rais Dkt.Mwinyi amesema, nia ya Serikali ni kuufanya uwanja huo uwe na sifa za Kimataifa na kutoa huduma bora kwani wageni walikuwa wakipata kero kubwa wakati mwingine kukaa zaidi ya saa tatu wakati wa ukaguzi.
"Hivyo hii hatua ni nzuri, tunataka kuona mabadiliko katika uwanja wetu wa ndege,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Pia amezungumzia kuhusu vipimo vya UVIKO-19 kufanywa na taasisi binafsi nchini, ujenzi wa barabara za ndani kufanyika bila ya zabuni pamoja na hatua ya Serikali kuvitoa kwa shughuli za Uwekezaji Visiwa vidogo vidogo.
"Ni zaidi ya visiwa 10 ambayo tumeshavitoa kwa wawekezaji kati ya visiwa 52,dhamira yetu ni ile ile ya kuhakikisha tunawaleta wawekezaji ili wawekeze miradi mikubwa hususani Sekta ya Utalii ambayo itafungua fursa za ajira,kukuza uchumi na kuimarisha pato la Taifa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini,"amesema Rais.
Maeneo mengine ni kuhusu nyumba za maendeleo, uchimbaji wa mafuta, nyumba za Mji Mkongwe, viwanja vinavyotolewa na Serikali na kupanda bei kwa bidhaa.
Muungano
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, licha ya kero nyingi za Muungano kupatiwa ufumbuzi, lakini hazitakwisha kabisa kwa sababu yapo mambo yanayoibuka kulingana na mahitaji na matakwa ya wakati uliopo
Aidha, amesema mafanikio ni makubwa na katika kero zote zilizopo kwa sasa hakuna inayomyima usingizi.
“Changamoto nyingi zimeshafanyiwa kazi kwa kweli mambo yanaenda vizuri, tupo kwenye hatua nzuri zaidi, tumeshuhudia hata hivi karibuni zimeondoolewa karibu kero 11 zimebaki saba.
“Lakini niseme tu kwamba changamoto za Muungano hazitafika mwisho, kwa hiyo matatizo yatakuwa yanaibuka,lakini yanashughulikiwa,” amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi.
Mawaziri
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi akizungumzia utendaji usioridhisha wa baadhi ya viongozi amesema, ataendelea kufanya mabadiliko kila inapohitajika kwa sababu ya utendaji kazi wao huku akisema hata baraza la mawaziri linaweza kufanyiwa marekebisho wakati wowote kutokana na utendaji kazi wao.
“Nimekaa serikalini miaka 20, sijawahi kuona Baraza la Mawaziri linaanza mwanzo hadi mwisho, kwa hiyo kubaidlishwa kupo, anayefanya vizuri tutakwenda naye asiyefanya vizuri tutamuweka pembeni,”amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Taarifa zaidi kuhusu mazungumzo na Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi zitakujia mfululizo hapa DIRAMAKINI BLOG, endelea kufuatilia ufahamu zaidi.