NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, viongozi wote wa Serikali wakiwemo mawaziri, makatibu, wakurugenzi, watendaji na wengine watapimwa kwa utendaji kazi wao, hivyo wale ambao wataonekana hawawezi kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Nane itabidi wakae pembeni.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 11, 2021 katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar wakati akizungumza na wahariri wakiwemo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Zanzibar.
Akijibu moja ya swali aliloulizwa na washiriki wa majadiliano hayo kuhusu taarifa za kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, "Baraza ni kitu ambacho lazima kibadilike, hauwezi kuanza na baraza nalo la mwaka huu, pale tunapoanza ukamaliza na wote.
"Haiwezekani, kwa hiyo si kwamba tunapanga baraza, tuna 'monitor' (tunafuatilia) kila mtu anafanya nini? Yule ambaye anafanya vizuri ataendelea, yule ambaye hafanyi vizuri itabidi atupishe tuweke watu ambao wanafanya vizuri.
"Kwa hiyo watu wasiingie hofu kwamba kesho au kesho kutwa nitatangaza baraza,hapana. Ninachosema ni kwamba sisi tuna 'monitor' (tunafuatilia), kila mtu anafanya nini,lakini mimi nimekaa serikalini kwa miaka 20, sijawahi kuona baraza lililoanza likamaliza, hapa katikati watapungua.
"Hiyo ni kawaida, kwa sababu watu huwa wanapimwa kwa utendaji, wale ambao wanatenda vizuri wanabaki, wale ambao hawatendi vizuri inabidi wawapishe ambao watatenda vizuri.
"Kwa hiyo na hapa Zanzibar ni hivyo hivyo, tutakwenda, tukiona kwamba sasa kuna watu yale majukumu yao hayatekelezwi vizuri,tutafanya mabadiliko, na hii haihusishi baraza peke yake, ni wote, makatibu wakuu ni hivyo hivyo,wakurugenzi ni hivyo hivyo, watu wote ni hivyo hivyo ikiwemo katika halmashauri zetu. Tutaendelea kupanga watendaji kwa mujibu wa utendaji wao hapa nchini,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Mwelekeo
Amesema, Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Nane imejiwekea vipaumbele vyake ambavyo ni pamoja na kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
Ndiyo maana alipoingia madarakani alichukua juhudi za haraka kukutana na wenzake na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imetoa mwelekeo chanya katika kuwatumikia wananchi Zanzibar ili kuwaletea maendeleo.
"Hivyo, baada ya hatua hiyo, kilichofuata sasa ni uwajibikaji.Kila mmoja anawajibika katika nafasi yake ili kuhakikisha tunawaletea wananchi maendeleo kwa haraka,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Amebainisha kuwa, kipaumbele kingine katika Serikali yake ya Awamu ya Nane ni kuhakikisha yanakuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi ambao watawekeza katika vitega uchumi ambavyo vitatoa ajira kwa vijana na kuchangia pato la Taifa.
"Ndiyo maana Serikali imechukua juhudi za makusudi za kuimarisha Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
"Utendaji wa ZIPA umeimarika baada ya kuanzishwa kituo kimoja kinachotoa huduma za uwekezaji (one stop centre), kikihusika na utoaji wa vibali vya ukaazi, ujenzi, usajili wa kampuni, masuala ya kodi pamoja na mazingira. Kwa sasa mwekezaji anaweza kupata kibali cha uwekezaji ndani ya siku tatu endapo atakamilisha vyema taratibu kabla kwenda kituoni,malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane ni kuhakikisha, mwekezaji anakamilisha usajili huo ndani ya siku moja,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Pia amesema, jambo lingine ni kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu bora, afya, maji na nyingine nyingi ili wananchi waweze kuzipata kwa karibu zikiwa na ubora na kwa wakati.
Vile vile amesema, Serikali imejizatiti kukomesha matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya, vitendo vya udhalilishaji, dhuluma, migogoro ya ardhi na mengine nchini.
Uchumi wa Buluu
Akizungumzia kwa upande wa Uchumi wa Buluu, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali yake imejipanga vilivyo kujenga Zanzibar mpya kupitia uchumi wa kisasa ambao unatokana na uwepo wa bahari.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Uchumi wa Buluu unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbalimbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.
"Hivyo, uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu, ndiyo maana lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujenga bandari kubwa za kisasa ambazo zitatoa huduma kwa wavuvi na kuchangia kukuza uchumi wa Zanzibar,"amesema.
Amesema kuwa, Uchumi wa Buluu ni fursa moja wapo kuu katika kuwezesha upatikani wa ajira kwa vijana, kukuza pato la Taifa na kutoa fursa kubwa kwa wawekezaji kuwekeza katika miradi mikubwa ambayo ina matokeo makubwa kwa Taifa.
Uchumi wa Buluu unaziguza moja kwa moja sekta wezeshi za ajira kwa vijana ikiwemo utalii, mafuta na gesi, uvuvi, bandari, kilimo cha zao la mwani.
"Hivyo Serikali inafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kupitia Uchumi wa Buluu, vijana wanapata ajira, wakulima wa mwani wananufaika, wavuvi wananeemeka kwa kupatiwa zana za kisasa ili waweze kwenda umbali mrefu ambapo watapata samaki wa kutosha, vivyo hivyo katika ujenzi wa hoteli za kitalii, mafuta na gesi,"amesema.