NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa vSamia Suluhu Hassan amesema Uhuru wa Tanganyika ulikuwa chachu na mchango muhimu katika kuwezesha mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12,1964.
Ameyasema hayo Desemba 8, 2021 wakati akilihutubia Taifa ikiwa ni saa chache kabla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, 1961.
Mheshimiwa Rais amesema, matukio hayo mawili yaliyotangulia Muungano ndiyo yaliweka msingi imara wa nchi na Taifa imara la sasa, lenye amani, mshikamano na umoja miongoni mwa watu wake.
Amesema, kwa msingi huo tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kutujaalia uzima wa kuiona siku hii ya kihistoria katika Taifa.
Rais Samia amesema, kwa takwimu za watu, Watanzania takribani milioni 2.52 kati ya hao milioni 59 waliopo leo sawa na asilimia 4.3 ya watu wote ndiyo walikuwa wamezaliwa kabla ya Desemba 9, 1961.
Amesema, hiyo ina maana kuwa sehemu kubwa ya Watanzania wanaoadhimisha miaka 60 ya Uhuru ifikapo Desemba 9, 2021, wanaweza wasipate tena fursa ya kuadhimisha makumi mengine yajayo ya maadhimisho haya.
“Tunaoshuhudia siku hii ya leo, tujione ni kati ya wenye bahati. Takwimu hizi zinatuambia jambo lingine muhimu kuwa Watanzania wengi waliopo leo si tu hawakuwepo wakati wa Uhuru bali tu hawakuyaishi madhila ya ukoloni na matokeo yake,” amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Rais Samia amesema, mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya Uhuru yamebebwa na utawala wa demokrasia na sheria.
Amesema, wakati wa uhuru kulikuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao, baadaye mwaka 1962 ulifutwa ili kujenga umoja na mshikamano wa nchi kwanza.
Baadaye mfumo huo ulirejeshwa tena mwaka 1992 baada ya nchi kupiga hatua kubwa katika utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi.
“Tangu kurejea mfumo wa vyama vingi, vipo vyama 16 vilivyosajiliwa na 17 vinavyoomba usajili wa muda. Tumekuwa na mfumo bora unaoheshimiwa na imara wa kuweka viongozi madarakani kupitia chaguzi za kila baada ya miaka mitano,” amesema Rais Samia.
Aidha, Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, wananchi wamekuwa na haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka na kuchaguliwa pindi wanapotaka kushika madaraka katika ngazi tofauti za uongozi.
“Wakati wa uhuru nchi ilikuwa na wabunge 80 ukilinganisha na nafasi za wabunge 393 na waliopo ni 391, kati ya hao wanawake ni wabunge 143 na wanaume ni 248. Kama nchi imeendelea kulinda na kuheshimu na kulinda haki za msingi za binadamu na watu kwa kuweka mifumo ya kuwezesha wananchi kutoa maoni kwa uhuru bila kubugudhiwa,” amesema Rais Samia.
Pia kuhusu Uhuru wa vyombo vya habari, Rais Samia amesema, vimeendelea kuwa huru na hadi sasa magazeti na majarida yaliyosajiliwa nchini yamefikia 270, redio 198, redio za mtandaoni zaidi ya 200, blog 120, televisheni 51, televisheni za mtandao zaidi ya 500 ikilinganishwa na chombo kimoja wakati wa uhuru.
Mheshimiwa Rais Samia amesema, Tanganyika imekuwa na safari ndefu baada ya Uhuru ikiwemo kutoka katika kundi la nchi maskini hadi kufikia uchumi wa kati wa chini.
Amesema, safari ya kutoka uchumi wa kati wa chini kwenda uchumi wa katikati na baadaye uchumi wa juu si ndefu sana huku akisema kazi inayofanyika itakuwa ni chachu ya kufika huko
Mheshimiwa Rais Samia amewataka watumishi kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na Muungano wetu.
Sambamba na kuendelea kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu na kufanya mageuzi ya kiuchumi kila inapolazimu kuendana na kasi ya uchumi wa Dunia.
Pia amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na kuyalinda kwa wivu mkubwa ili kurithisha vizazi vijavyo nchi yenye neema kama ilivyopokelewa kwa vizazi vilivyotangulia.
Mheshimiwa Rais Samia amesema, Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 inaelekea tamati huku uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa asilimia nane.