Serikali Kiteto wajipanga kukabiliana na migogoro ya ardhi kabla ya shughuli za kilimo

NA MOHAMED HAMAD

KATIKA kuelekea msimu wa kilimo, Serikali wilayani Kiteto mkoani Manyara imejipanga kukabiliana na migogoro ya ardhi ambayo mara kadhaa imekuwa ikijitokeza na kusababisha madhara makubwa kwa wakulima na wafugaji.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Al Haji Batenga akizungumza kwenye kikao cha maendeleo ya wilaya DCC.

Wakulima na wafugaji wilayani Kiteto hujeruhiana na hata wakati mwingine kupoteza maisha katika kugombea ardhi, hivyo Serikali imeanza mkakati kukabiliana na migogoro hiyo.

Katika kipindi cha kilimo wakulima huitumia ardhi kwa kilimo wakati wafugaji wao huwa wanaitumia ardhi kufugia, hivyo kusababisha mvutano ambao madhara hutokea baina ya pande hizo.

Akizungumza kwenye kikao cha Ushauri Wilaya ya Kiteto (DCC), Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Al Haji Batenga aliagiza Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na vijiji watatue migogoro hiyo mara moja katika maeneo yao kabla ya shughuli za kilimo kuanza rasmi.

Alisema, migogoro mingi Kiteto inatokana na baadhi ya viongozi wa vijiji kuifanya kuwa vyanzo vya mapato yao na kusema kamwe hatolifumbia macho, Kiongozi yoyote atakayehusika, sheria itafuata mkondo wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto, John Nchimbi alisema, ataanza kuwashughulikia Maafisa Watendaji wa vijiji na kata watakaokuwa vyanzo vya migogoro hiyo akisema, kipimo cha mtumishi kama anawajibika ni pamoja na uwepo wa amani katika eneo lake.

Bakari Soka (Mzee maarifu) Kiteto alisema jamii ya wafugaji imekuwa ikitumia udhaifu wa baadhi ya watumishi wa Serikali kwa kutowajibika na kusababisha madhara makubwa kwa wakulima kujeruhiwa na kuharibiwa mazao yao.

"Mhe Mkuu wa Wilaya hapa maeneo mengi yana mipango ya matumizi Bora ya Ardhi kwanini watu hawachukuliwi hatua wanapovuja, kwanini migogoro hii inaachwa iendelea ili hali kila eneo lina mipango yake," alisema.
Ukitaka kuyaona haya angalia malalamiko ya wakulima juu mipango hiyo, wafugaji wanalisha mifugo mashambani wakati wa usiku..wanachunga mchana kweupe kama mkulima kakosea kwanini asikamatwe na kufikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake kwanini mazao yake yanaharibiwa na kupigwa? Alihoji Bakari.

Naye Shukumu Moringata alisema tatizo lililopo kwa wakulima ni kulima mpaka maeneo ya wafugaji, hivyo kusababisha mifugo kukosa maeneo ya kuchunga

Kila mahali ni kilimo sasa unataka mifugo ichunge wapi mpaka hata barabara zimelimwa ipite wapi naomba Sheria ifuate mkondo wake ili pande hizo zibaki salama alisema Shukumu.

Mkuu wa TAKUKURU Kiteto, Venance Sangawe, katika kikao hicho alisema rushwa imetawala katika maeneo yenye migogoro ya ardhi na kuwataka viongozi hao kuwa makini kwani madhara ni makubwa ndani ya jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news