Serikali yasisitiza itaendelea kuvilinda,kuvisimamia viwanda vya kubangua korosho,RC Kunenge afafanua

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa, Serikali itaendelea kuvilinda na kuvisimamia viwanda vya ubanguaji wa zao za korosho vilivyopo mkoani humo ili viweze kufanya kazi vizuri na iliyokusudiwa.
Kunenge, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kiwanda cha ubanguaji Korosho cha Uvuki na Alphalerust vilivyopo Kibaha Mjini.

Kunenge amesema kuwa, kufanyika kwa ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka Korosho zote za Mkoa wa Pwani lazima zibanguliwe na viwanda vya Pwani.

Amesema,kutokana na kauli hiyo aliona ni vyema kuchukua hatua ya mara moja kufanya ziara katika viwanda hivyo huku akisema kuwa lengo la ziara ni kutaka kujua changamoto mbalimbali zilizopo viwandani humo.

Kunenge amesema kuwa, ukiachia mbali changamoto zilizokuwepo viwandani humo lakini pia ziara hiyo pia imeangalia juu ya masuala ya vibali,uwezo wa kuzalisha,upatikanaji wa malighafi,na teknolojia inayotumika.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ( kushoto) akizungumza na mmiliki wa kiwanda cha ubanguaji Korosho cha Alphalerust kilichopo Tanita Kibaha Mjini Chirag Patel,katika ziara aliyoifanya kiwandani hapo.

"Nimeona nivitembelee viwanda vya ubanguaji zao za Korosho kwa ajili ya kutaka kuhakikisha maelekezo ya Rais Samia yanafanyiwa kazi na hivyo kufikia malengo yake ya kuhakikisha Korosho zote zinabanguliwa na viwanda vya Pwani,"amesema Kunenge.

Amesema,ataendelea kukutana na wamiliki wa viwanda hivyo ili kujua zaidi changamoto zao na kwamba kikubwa ni kuvisimamia ili kuhakikisha vinafanyakazi vizuri na iliyokusudiwa.

Aidha, Kunenge ameongeza kuwa anataka kuona wakulima wa zao hilo wanalima zaidi lakini kilimo chao kiendane na mazingira bora hasa katika kupata viwanda vya uhakika na masoko ya uhakika.

Amesema kuwa,msimu uliopita Pwani imezalisha Korosho zaidi ya Tani 7000 lakini msimu huu uzalishaji utaongezeka mpaka kufikia Tani 11000 na kwamba lazima maandalizi yake yafanyike mapema.

Meneja uendeshaji wa kiwanda cha Alphalerust kilichopo eneo la Tanita Kibaha Mjini, Chirag Patel amesema, kiwanda chake kinaendelea vizuri licha ya uzalishaji kuwa chini ya kiwango.

Patel amesema kwa sasa wanazalisha Tani tatu mpaka nne kwa siku kwakuwa uwezo wa mashine zilizopo ni mdogo lakini wapo katika mpango wa kupata mashine mpya.

Amesema,mashine mpya kubwa zinaingia Januari 2022 ambazo kwa kiasi kikubwa zitaongeza uzalishaji kiwandani hapo kutokana Tani 8 mpaka 10 kwa siku na Tani 3000 hadi 4000 kwa mwaka.

Hata hivyo,Patel ameiomba Serikali itoe kibali cha kuanza kununua Korosho mapema kabla ya mnada ili waweze kupata Korosho nyingi zitakazoendana na mahitaji ya kiwanda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news