NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt.Leonard Akwilapo ametoa agizo kwa wathibiti wa ndani wa elimu nchini kufanya msako kwa watakaofundisha wanafunzi masomo ya ziada katika kipindi cha likizo.
Amesema,itatolewa barua kwa shule zote za Serikali na binafsi ili kuweka msisitizo wa utekelezaji wa agizo hilo ambalo hivi karibuni Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Ummy Mwalimu alisema kuwa wakati wa likizo wanafunzi wasisome bali wapumzike.
Dkt.Akwilapo ameyasema hayo Desemba 7, 2021 alipokuwa akifungua mafunzo ya uthibiti wa ndani kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Katibu Mkuu huyo amesema kuwa, wathibiti wa ndani wa elimu nchini watafanya msako kuwabaini watakaofundisha wanafunzi wakati wa likizo.
Amesema, maofisa elimu hao wamesoma somo la saikolojia na wanajua umuhimu wa mapumziko katika makuzi ya mtoto, hivyo hawapaswi kufunbia macho vitendo hivyo.
"Kupitia hadhira hii nawaagiza maofisa udhibiti kipindi hiki cha likizo hakikisheni mnafanya msako kuwabaini wanaokiuka agizo hili la Serikali la kuwataka watoto wapumzike na katika kuweka msisitizo hilo tutazipa barua shule zote.
"Ni muhimu kufuata ratiba za mihula ya masomo, kwani kumeibuka siku hizi makamishna wengi wa elimu huko mashuleni mpaka wanasiasa, nasema kamishna ni mmoja tu wa elimu nchi hii anayepanga ratiba za masomo, hivyo ni vema ikafuatwa,"amesema Dkt.Akwilapo.
Pia amesema, hata tabia ya kuwahamsha watoto saa 10 usiku kusoma si sawa na badala yake wanajikuta wanakariri badala ya kutafakari kile walichofundishwa shuleni.