NA HADIJA BAGASHA
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu, Mhe. Ummy Nderiananga amesema, Serikali imetoa shilingi bilioni nane kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu nchini.
Mheshimiwa Ummy ameyasema hayo katika kongamano la kuelekea Siku ya Watu wenye Ulemavu duniani ambayo kitaifa itafanyika jijini Tanga ambapo amezungumzia kuhusu fedha kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu
Hassan kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi.
Amesema, fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo
hivyo vipya utakwenda sambamba na kukarabati vilivyopo na kwa kuanzia
ikiwemo kujenga chuo Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Mkoa wa Songwe katika
Halmashauri ya Mbozi.
Aidha, amesema chuo kingine kitajengwa
wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ambavyo ni vyuo vipya na michoro yake
imekwisha ambapo walikuwa wanashirikiana na wahandisi na wamemaliza.
“Niwaambie kwamba Mheshimiwa Rais ameweka fedha tayari ipo Hazina
wanasubiri michoro ipelekwe na tumepiga hatua na Rais analithamini sana
kundi letu na vyuo vyetu vilivyobakia vyote vikae kwenye mfumo mmoja
vipendekeze,"amesema.
“Nataka niwaambie hapa Tanga kuna chuo cha
Masiwani cha watu wenye ulemavu na Serikali inaboresha vyuo vyote na
Rais ametoa fedha milioni 4 kupitia TAMISEMI kujenga mabweni ya
wanafunzi wenye ulemavu kwenye shule za Msingi yatajengwa mabweni 50 na
hapa Tanga tutajenga mabweni mawili yameeshaanza na yanaendelea
vizuri,"amesema.
Hata hivyo, alisema wameamua kufanya hivyo
kutokana na kwamba wanafunzi wenye ulamavu wanapata shida ya umbali na
Rais ameliona hilo na ametoa fedha hizo ili wanafunzi wakae shuleni
wasome na kuondokana na changamoto ambazo walikuwa wanakabiliana nazo
awali.
“Tunampongeza Rais wetu Samia Suluhu na tuendee kumuunga mkono kwani amedhamiria kuhakikisha changamoto zinazowakabili watu wenye ulamavu zinapatiwa ufumbuzi,”amesema.
Naibu Waziri huyo amelitaka Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) kuacha fitina, figisu na migogoro kwani haina tija na itapelekea kuwachelewesha kufikia malengo yao.a
Naibu waziri Nderiananga amesema, kuna watu mabingwa wa kutengeneza makundi kwenye vyama vya wenye ulemavu na kusababisha kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Naibu waziri Ummy amesema ni lazima wabadilike na kuondokana na dhana ya kuipa nafasi migogoro badala yake wasaidiane ili waweze kutimiza malengo yao kutokana na kwamba hakuna kitu kinachochelewesha kufikia malengo yaoe kama hicho ikiwemo kushirikiana kwa pamoja na kupendana wao wenyewe.
“Ndugu zangu pendaneni, saidianeni uongozi ni kuchukuliana kusaidiana acheni chokochoko ukinichokonoa mimi nikadondoka utadondosha na wengine, hivyo niwasihi achaneni na mambo hayo badala yake shikaneni,"amesema.
Washiriki wa kongamano hilo akiwemo Tongi Mwanjala ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (SHIVIAWATA) na Elieza Robert ambaye ni mjumbe wa bodi wamesema, fedha hizo zitasaidia watu wenye ulemavu kujifunza masuala mbalimbali na kujikwamua kiuchumi.
Siku ya watu wenye ulemavu duniani huadhimishwa kila ifikapo Desemba 3 wakati ambao watu wenye ulemavu wanakutana na kupata nafasi ya kupaza sauti zao dhidi ya changamoto zinazowakabili.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku hiyo.