NA FRESHA KINASA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Khamis Hamza Chillo amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa Askari na Watumishi watakaobainika kushiriki kuharibu ushahidi ama kuwalinda watuhumiwa wa makosa ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia ili wasitiwe hatiani.
Naibu Waziri huyo ameyasema hayo Desemba 10, 2021 wakati akifungua mkutano Mkuu wa Mwaka wa siku mbili wa Maafisa, Wakaguzi na askari wanaofanya kazi Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar ambao unafanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwanza iliyopo Jijini Mwanza.
Mheshimiwa Khamis amesema askari wanapaswa kuzingatia weledi na kutenda haki pindi wanaposhughulikia upelelezi na uchunguzi wa matukio mbalimbali ya Ukatili wa Kijinsia ili kusaidia watuhumiwa kutiwa hatiana na sio kuharibu ushahidi na pia madaktari ambao hupewa jukumu la kufanya uchunguzi wa kitaalamu amesema wanawajibu wa kutoa ripoti za kweli na sio kupindisha ukweli.
"Kila mmoja atimize wajibu wake, kama ni daktari umeletewa mtoto aliyefanyiwa ukatili afanye uchunguzi na kutoa ripoti ya haki, Kama ni polisi anafanya uchunguzi wa kesi asishiriki kutetea mhalifu tukibaini mtumishi wa Serikali yuko sehemu ya kurudisha nyuma juhudi za serikali kumaliza ukatili hakika tutashughulika naye nia ya Serikali ni kumaliza ukatili wa kijinsia,"amesema Mheshimiwa Khamis.
Aidha, Naibu Waziri huyo amewataka Maafisa na askari wa Dawati la Jinsia na Watoto nchini kuendelea kutoa elimu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia Katika maeneo yao bila kuchoka na kwamba dhamana waliyonayo inatija Katika kuimarisha Ustawi bora wa maisha ya wananchi. Huku akisisitiza Wazazi na walezi kuendelea kuwa walinzi wa watoto wao kwa kufuatilia mienendo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti linalojishughulisha na mapambano ya Ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema Shirika hilo limeendelea kufanya kazi kwa Karibu na Maafisa wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Wilaya ya Serengeti ikiwemo kutoa elimu kwa Jamii juu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia na kuwawezesha wanawake kwa kuwapa simu Janja zinazosaidia kuripoti matukio hayo katika maeneo yao.
Rhobi amesema kuwa, mapambano ya Ukatili wa Kijinsia yanapaswa kufanywa na kila mwananchi ikiwemo kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo bila kuwaonea aibu hatua ambayo itasaidia kwa kiwango kikubwa kutokomeza ukatili wa Kijinsia.
Faidha Yusuph Suleiman ni Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ambapo amesema dawati hilo limeendelea na Majukumu mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya Ukatili wa Kijinsia na kwamba Wananchi wameendelea kupata uelewa mpana sambamba na kuwa na mfumo wa kurekodi matukio mbalimbali ya Ukatili wa Kijinsia.
Ameongeza kuwa, Dawati hilo linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa magari maalumu ya kufanyia kazi hasa kwenda Vijijini, vifaa vya ofisi na baadhi ya maeneo kutokuwa na Ofisi maalumu.
Aidha, Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly amekabidhi tuzo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro iliyopokelewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanz Ramadhan Ng'anzi pamoja na kwa Maafisa, Wakaguzi na askari 18 wanaofanya kazi Dawati la Jinsia na Watoto katika kutambua juhudi zao za kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneo yao.