NA ANGELA MSIMBIRA-OR TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali imepeleka Sh bilioni 109 kwa ajili ya kujega shule 234 zitakazojengwa kwenye majimbo yote 214.
Ameyasema hayo wakati wa kuelezea mwelekeo wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa baada ya ya kuelezea mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema, shule hizo ni miongoni mwa shule 1,000 ambazo zimepangwa kujengwa katika kata zisizo na shule za sekondari na zenye msongamano mkubwa wa wanafunzi kutokana na fedha za mkopo nafuu wa sh. trilioni 1.5.
Ameendelea kufafanua kuwa, fedha hizo zimepagwa kujenga shule 234 za kata katika majimbo yote 214 na shule 20 kwenye halmashauri ambazo zina shule zenye uwiano mkubwa wa wanafunzi darasani.
“Nitumie fursa kuelekeza kuwa fedha hizi zitumike kuanza ujenzi wa madarasa 8, vyumba vitatu vya maabara ya masomo ya sayansi na matundu ya vyoo,”ameelekeza Waziri Ummy.
Kuhusu shule za sayansi za wasichana kila Mkoa, Waziri Ummy amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI imepeleka shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kujenga shule 10 za wasichana.