NA MWANDISHI MAALUM
TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imewatoa Watanzania wasiwasi kuhusu shehena inayosemekana kuwa na viasili vya mionzi iliyokusudiwa kuingizwa nchini kupitia Bandari ya Mombasa nchini Kenya.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Desemba 22,2021 na Dkt.Justin E.Ngaile ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAEC.
"Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ilipata taarifa kupitia vyombo
mbalimbali vya habari vya Kenya kuhusu shehena yenye namba TCKU3337296
inayosemekana kuwa na viasili vya mionzi ya nyuklia iliyokuwa kwenye meli MV
SEAGO PIRAEUS VOY 174S.
"Shehena hiyo inasemekana ilikuwa ikisafirishwa (Transshipment) kuja Tanzania kupitia Bandari ya Mombasa.
Baada ya kupata taarifa hiyo TAEC iliwasiliana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mionzi ya Nyuklia Nchini Kenya (Kenya Nuclear Regulatory Authority-KNRA) ili kubaini ukweli wa taarifa hizo.
"Tarehe 21 Disemba 2021, KNRA ilithibitisha taarifa hizo ni za kweli na tayari mamlaka ilichukua hatua stahiki na shehena kuamriwa kurejeshwa ilikotoka. Kwa taarifa za leo Jumatano tarehe 22 Disemba 2021, saa sita na nusu usiku 00:30 (00:30 LT(UTC+4)) meli hii ilikuwa imetia nanga nchini Oman katika Bandari ya Salalah.
"TAEC inapenda kuwatoa hofu watanzania wote kuhusiana na taarifa ya tukio hilo kwani shehena hiyo haikufika nchini. Hata hivyo, Serikali iko macho na imejipanga vyema katika udhibiti wa uingizaji vyanzo vyote vya mionzi kupitia Bandari na sehemu zote za mipaka nchini.
"Pia tunawafahamisha wananchi kuwa sheria, kanuni na taratibu zote za matumizi salama ya mionzi ya nyuklia nchini zinafuatwa ili kuwakinga na madhara yatokanayo na vyanzo vya mionzi,"imefafanua taarifa hiyo.
TAEC inaendelea kutoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kufuata sheria na taratibu za uingizaji na utoaji wa bidhaa zao ikiwemo kupata vibali vinavyoruhusu uingizaji wa vyanzo vya mionzi na bidhaa za vyakula nchini ili kulinda na kuhakikisha usalama wa wananchi na masoko ya nje.
"Mionzi kwa kwa matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa"
(Picha na TheStandard).