TANESCO wanafanya sehemu yao, wananchi na sisi tuwajibike sehemu yetu kwa nishati ya kudumu

VIONGOZI wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wameendelea kuumiza vichwa.
Kwao usiku ni kama mchana, mvua yao, jua lao,pengine wakati mwingine kuonana na familia imekuwa mara chache chache sana, sababu kuu ikiwa ni kuhakikisha kuanzia Kanda ya Kusini, Mashariki,Magharibi, Kaskazini na kwingineko panakuwepo nishati ya uhakika ya umeme.

Ndiyo maana wametazama mbele zaidi ili kuona ni kwa namna gani wanafanyia kazi changamoto ya upungufu wa umeme inayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Miradi ipo mingi, imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa lakini katika haya, TANESCO wameona kuna umuhimu wa kuanza utekelezaji wa miradi ya upanuzi wa Kinyerezi I utakaozalisha Megawati 185 na Ubungo III utakaozalisha Megawati 112.

DIRAMAKINI BLOG, tunaamini hii ni hatua njema na muhimu zaidi kwa mustakabali wa huduma endelevu na za uhakika za nishati ya umeme nchini.

Tumemsikia na kumwelewa Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande siku ya Desemba 15, 2021 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 51 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi unaoendelea mkoani Morogoro akisisitiza kuwa,wanaendelea kuchukua hatua na kuongeza jitihada za kuhakikisha unapotokea upungufu wa mvua unaoathiri uzalishaji basi athari za moja kwa moja za upungufu wa umeme zisijitokeze nchini.

Maono hayo ni dhairi kuwa, yamebeba matokeo chanya ambayo yana tija si tu kwa jamii bali kwa Taifa na wawekezaji ambao wanategemea asilimia kubwa ya nishati ya umeme nchini kwa ajili ya uzalishaji.

Haya yote yanaweza kutimia iwapo, sisi binadamu tutabadili mienendo yetu na kuhakikisha katika maisha yetu ya kila siku tunayapa thamani mazingira yetu kwa kutunza vyanzo vikubwa kwa vidogo vya maji.

Kuonyesha ukali na pengine kuwachukulia hatua za haraka ambao kwa kujua au kutokujua wamekuwa mstari wa mbele kukata miti ovyo, na tuwe mabalozi wema katika upandaji wa miti katika kila kona ya nchi yetu.

Wataalamu wanasema, tiba ya kwanza katika kuyakabili mabadiliko ya tabia nchi ni kuhakikisha upandaji na usimamizi wa miti ambayo ndiyo chanzo kikuu cha mvua inayotuwezesha kupata nishati ya umeme kupitia vyanzo elekezi inakuwa kipaumbe cha kwanza.

Sisi tukiwajibika katika utunzaji wa vyanzo vya maji, utunzaji wa mazingira na kupanda miti ya kutosha halafu mvua zikawepo za kutosha huku tukilinda kwa hali na mali, Miundombinu ya TANESCO dhidi ya wahujumu, tukikosa umeme, TANESCO watakuwa na la kujibu.

Lakini tukiendelea kudhoofisha vyanzo hivyo, kukata miti ovyo na kuharibu Miundombinu ya TANESCO tukakosa umeme, huku tukiwanyooshea kidole. Tutakuwa hatuwatendei haki.

DIRAMAKINI BLOG inaendelea kuamini kuwa, juhudi za viongozi wa TANESCO chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Maharage Chande wanaweza kutufikisha mbali ikiwa watapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa kila mmoja wetu.

Tumeona tayari mkataba umesainiwa kwa Mradi wa Kinyerezi I kwa ajili ya upanuzi na kufikia mwezi Aprili 2022 ambapo kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji, kituo kitaanza kuingiza kwa awamu Megawati 60 kwenye Gridi ya Taifa.

Huku mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere utakaozalisha Megawati 2115 utakapokamilika ukitarajiwa kuondoa tatizo la uhaba wa umeme nchini.

Akizungumzia suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na ukame uliochangia mitambo ya maji kushusha uwezo wa uzalishaji umeme, amesema hali imeanza kuwa nzuri kwa sasa japo bado tatizo halijakwisha kabisa.

Mkurugenzi Mtendaji amebainisha kuwa, maeneo ya Kilombero, Morogoro mvua zimenyesha na kwa mfano bwawa la Kidatu ambalo linategemea maji kutoka Mtera na mito midogo ukiwemo Iyovi, kina cha maji kimeanza kuongezeka. Hii ikiwa ni hatua njema.

Amesisitiza wateja watarajie hali ya umeme kuimarika zaidi na kwamba kutakuwa na mifumo itakayomuwezesha mteja kufanya maombi ya umeme bila kufika kwenye ofisi za TANESCO.

Ni imani yetu, ushirikiano wa kutosha baina ya wananchi na TANESCO utawezesha shirika hilo la umma kuyaangaza maisha yetu kupitia nishati ya umeme.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news