Uganda yatoa kichapo kwa Tanzanite, Taifa Stars Siku ya Uhuru Tanzania Bara

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

TIMU ya taifa ya wasichana ya Uganda (Crested Cranes) imeichapa Tanzanite ya Tanzania chini ya Umri wa miaka 20 (U20) bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki.

Ni mtanange ambao umepigwa Desemba 9, 2021 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Mtanange huo ulikuwa ni sehemu ya sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizofanyika Kitaifa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Bao la Crested Cranes limefungwa na Khadija Nandago dakika ya 18 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Janet Simba.

Ni kufuatia mpira wa adhabu wa Samalie Nakacwa kutoka upande wa kulia baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu na Protasia Mbunda.

Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetoka patupu katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Uganda Cranes.
Taifa Stars ilikubali kufungwa magoli 2-0 katika mchezo huo wa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Mitanange hiyo ya Desemba 9, 2021, Taifa Stars ambayo inanolewa na kocha Kim Poulsen ilikuwa inakikosi cha wachezaji wengi ambao hawapati nafasi sawa na Uganda ambapo ilimaliza kipindi cha kwanza wakiwa sare tasa kabla ya ngwe ya pili iliyotoa pigo.
The Cranes mabao yao yamefungwa na Ivan Masaba dakika ya 71 kabla ya dakika ya 90 Joseph Bright kufunga goli la kushtukiza kufuatia walinzi wote wa Taifa Stars kupanda mbele kushambulia kwenye mpira wa kona, kisha kipa Metacha Mnata kufanya makosa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news