Uzazi wa mpango ulivyo na nguvu ya kuimarisha afya ya mama, mtoto na maendeleo katika jamii

NA GODFREY NNKO

MAAMUZI ya hiari ya mtu au wenza juu ya ni wakati gani waanze kuzaa,watoto wangapi wazae, wapishane kwa umri gani na lini waache kuzaa yanatajwa kuwa moja wapo ya hatua muhimu katika kumuhakikishia mama na mtoto usalama wa afya zao ikiwemo ushiriki chanya wa maendeleo ya kijamii na uchumi nchini.
Uhusiano mwema baina ya wanawake, wanaume katika familia ni jambo la faraja ambalo linawapa nafasi wapendanao kufanya uamuzi sahihi kwa mustakabali wa familia yao hususani matumizi ya huduma za uzazi wa mpango. (Picha na Maktaba ya TMEPiD).

Uhiari huo ambao kwa maana nyingine tunazungumzia uzazi wa mpango unamuhusu yoyote mwenye umri wa kuzaa au anatarajia kufikia umri huo.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa, uzazi wa mpango ni muhimu kwa wanawake na wanaume,watu waliooa na kuolewa au ambao hawajaoa wala kuolewa na watu wenye watoto au bado hawajapata watoto.

Meneja wa Utetezi wa Shirika la Tanzania Communication and Development Centre (TCDC), James Mlali anasema kuwa, huduma za uzazi wa mpango ni muhimu zaidi katika kuboresha afya ya mama, afya ya mtoto ikiwemo kuleta maendeleo kwa ujumla.

Mlali anasema, kwa umuhimu huo, juhudi zinapaswa kufanywa ili kuongeza huduma hizo nchini kuanzia maeneo yote ya vijijini na mijini.

Ameyabainisha hayo katika Semina iliyohusu Umuhimu wa kuwa na Mbinu Jumuishi za Soko la Huduma za Uzazi wa Mpango Zinazopatikana kwa Urahisi na kwa kila Mwenye uhitaji, kwa Ufanisi na kwa njia Endelevu nchini.

Semina hiyo ya Desemba 14 hadi 16, 2021 ambayo iliwakutanisha pamoja wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ilifanyika mjini Morogoro ambapo iliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kukuza ushiriki wa wanaume katika Afya na Haki za Ujinsia na Uzazi (SRH&R), afya ya mama na mtoto pamoja na kukuza usawa wa kijinsia katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi la Tanzania Men as Equal Partners in Development (TMEPiD).

Mradi ambao umefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Idadi ya Watu (UNFPA) nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Mlali, TCDC,TMEPiD pamoja na wadau wengine ni watekelezaji wa mradi wa uzazi wa mpango nchini, ambao ni wa utetezi wa uzazi wa mpango.

"Huduma za uzazi wa mpango nchini, hali inaridhisha, lakini bado kuna haja ya kufanya kazi zaidi,ili tuweze kupiga hatua, kulingana na taarifa rasmi za afya na idadi ya watu za mwaka 2015 hadi 2016 ya Tanzania Demographic and Health Survey, tunaona kuwa watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango walifikia asilimia 32 katika kila asilimia 100, ambacho ni kiwango kidogo, hawajafikia hata theluthi au ni kama theluthi.

"Taarifa zinazotokana na matumizi ya kila mwaka zinaonyesha kuwa, kufikia 2020 idadi hiyo ilikuwa imefikia asilimia 41 na tuna malengo ya kuhakikisha watumiaji hao wanafikia asilimia 47 mwaka 2023, kwa hiyo unaona namna ambavyo tunapaswa kufanya kazi zaidi ili watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango waweze kuongezeka nchini.

"Na si tu waongezeke ili kuwa na idadi kubwa ya watumiaji, bali waongezeke kwa sababu huduma za uzazi wa mpango zina mchango mkubwa sana katika afya ya mama, afya ya mtoto na maendeleo kwa ujumla,"amesema Mlali.

Meneja wa Utetezi huyo amesema kuwa, idadi hiyo bado ipo chini, lakini ni vyema ikafanikiwa au kupita kutokana na umuhimu wa uzazi wa mpango.

"Lakini, pia taarifa za uzazi wa mpango katika Taifa letu zinaonyesha kuwa asilimia 30 ya mimba zote zinazotungwa nchini hazikutarajiwa,kutokana na matumizi madogo ya huduma za uzazi wa mpango nchini,kila mwaka karibu ya mimba zote zinazotungwa nchini, ni zile ambazo hazikutarajiwa, yaani wahusika hawakuwa wanapanga kuwa wazae, wengine wana mtoto mdogo, wengine umri umeenda sana, hana malengo ya kuzaa, lakini baada ya kushiriki tendo la ndoa au ngono wanajikuta wamepata mtoto.

"Pia tafiti za Ulimwengu mzima zinaonyesha kuwa, matumizi ya huduma za uzazi wa mpango yakifanyika vizuri, vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vinaweza kupungua kwa asilimia 44,na vifo vya watoto vinaweza kupungua kwa asilimia 35. 

"Kwa hiyo unaona kwamba ile idadi ya watu ambao wanakufa kutokana na changamoto ya uzazi inaweza kupungua sana, lakini pia idadi ya watoto ambao wanakufa katika umri mdogo inaweza kupungua sana.

"Na huo ni mchango mkubwa sana, kwa sababu Taifa linahitaji nguvu kazi kubwa, linahitaji wanawake wenye afya njema, linahitaji watoto wakue vizuri, wasikatishwe au maisha yao yasikatishwe, katika umri mdogo waweze kukuwa ili waweze kuwa sehemu ya nguvu kazi ya Taifa.

"Lakini kwa upande wa maendeleo kwa ujumla, huduma za uzazi wa mpango zina umuhimu mkubwa, kwa sababu ndizo ambazo zinasaidia familia, au watu binafsi kuamua idadi ya watoto ambao wanataka kuzaa, wawazae kwa wakati gani, wawaachanishe kwa umri gani kati ya mtoto na mtoto na hizo ndiyo kanuni bora kwa ajili ya afya mama na mtoto kwa maendeleo ya nchi.

Mlali anasema kuwa, Serikali inapaswa kuelekeza bajeti ya kutosha kwenye masuala yahusuyo uzazi wa mpango na inapaswa kupewa kipaumbele kikubwa, pia jamii ambazo zina fikira potofu kuhusu uzazi wa mpango zinapaswa kuachana na mawazo hayo.

Dkt.Maendaenda

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TMEPiD, Dkt.Cuthbert Maendaenda katika semina hiyo amesema kuwa, kila mtu ana haki ya kuamia ni wakati gani wa kuzaa na wakati gani si wa kuzaa.

"Taasisi yetu inahusika na utetezi na kuimarisha elimu afya ya uzazi katika jamii hasa ikiwalenga wanaume, kwa nini tunawalenga wanaume? Kwa sababu mbalimbali za kijamii, walikuwa ni kundi ambalo limewekwa pembeni. 

"Ukizungumzia mambo ya uzazi wa mpango zinawalenga wanawake, njia za uzazi wa mpango nyingi zinawalenga wanawake, huduma zinazotolewa mahali zinawalenga mama na mtoto, hivyo wanaume walikuwa wanakaa pembeni.Tukiangalia kimila, wanaume ndiyo wafanya maamuzi,kama ni mzazi mtoto apatikane lini, wapatikane watoto wangapi, maamuzi mara nyingi yanategemea wanaume, mila zimewapa hiyo nguvu au upendeleo.

"Kwa hiyo, kwa sasa tumejikita katika kujiimarisha kwenye utetezi wa afya ya uzazi wa mpango, tukisaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu hapa Tanzania, na kwa sababu tayari Serikali imekwishajiwekea malengo, Malengo ya Uzazi wa Mpango 2030, Serikali imepania kupanua matumizi ya huduma za uzazi wa mpango. 

"Na kupanua wigo wa wananchi kuweza kupata huduma za uzazi wa mpango, sasa katika kufanya hivyo, tukajikuta miaka mingi mtu akitaka kupata huduma ya uzazi wa mpango alipaswa kwenda kiliniki, usipokwenda kiliniki hauwezi kupata huduma,lakini pia kuna watu wengine wanapata shida ya kupata huduma, ukienda kiliniki au zahanati huduma hamna, kwenye jamii zingine ambapo vijana ambao ndiyo wapo kwa wingi zaidi, suala la uhusiano wamekuwa wakishindwa kufikia hizo huduma kwa sababu ya hofu ya wazazi wao, ndugu zao kwa sababu zinatolewa na watu wazima.

"Kwa hiyo kuna kundi kubwa sana, la Watanzania wanapotaka kuifikia huduma ya uzazi wa mpango wanashindwa kuifikia. 

"Kwa sasa tumekuja na Approach ya Total Market, katika hili tunachotaka ni huduma ya uzazi wa mpango zipatikane kila mahali, na kupitia wadau mbalimbali na si kwenda kliniki, tukiangalia huko miaka ya nyuma hata kupata huduma ya baba, mpira wa kiume au kondomu ilikuwa lazima uende kliniki, lakini kwa sasa ukitaka kondomu inapatikana kila mahali ikiwemo katika maduka ya rejareja.

"Kwa hiyo mtu hawezi kuacha kutumia kondomu, kwa sababu inapatikana kila mahali, na kwa sababu tunataka huduma nyingine zipatikane kila mahali za uzazi wa mpango ikiwemo katika famasi na maeneo mengine ili ziweze kupatikana kwa wingi hususani mashirika yanayotoa huduma hizo. Kwa hiyo mtu hawezi kuacha kutumia kondomu,"amesema Dkt.Maendaenda.

Amesema, tukifanya hivyo Taifa litapata faida nyingi kupitia upangaji salama wa uzazi wa mpango na hakutakuwa na kisingizio cha mtu kushindwa kuitumia huduma hiyo.

"Na kwa sababu hiyo tunataka huduma za uzazi wa mpango zipatikane kila mahali wakati wowote, kwa mfano katika maduka ya kutolea huduma za dawa kwa kuwapa mafunzo,mashirika kama TMARK ambao wapo mitaani, kwa hiyo, mwanamke au mwanaume akitaka huduma asilazimishwe, kama tumeweza kuzileta kondomu zikajaa, basi itafutwe njia nyingine ya kuhakikisha huduma zingine za uzazi wa mpango zinasambaa kila mahali.

"Lazima tutoe mafunzo, na kuhakikisha vikwazo vya kisera vinapatiwa ufumbuzi, kwa mfano duka la dawa muhimu haliwezi kutoa baadhi ya dawa za kuzuia mimba, sasa tunataka changamoto hiyo ipatiwe ufumbuzi ili kurahisisha mama anapotaka kwenda kuchukua vidonge vikiisha aweze kuvipata kwa haraka, vivyo hivyo kuondoa visingizio vya umbali, hivyo wengine kuacha kwenda kutumia huduma ya uzazi wa mpango,"amesema.

Pia amesema kuwa, idadi kubwa ya watu wanaoishi mijini wana uwezo hivyo inawezekana wakawa wanapatiwa huduma hizo kwa kugharamia ili kipato kitakachopatikana kiweze kupeleka huduma hiyo kwa wingi huko vijijini.

"Kwa hiyo itatupa faida kubwa ya kuhakikisha kule kijijini huduma zinajaa, lakini pia tunatetea kwamba haya mashirika ya bima na wenyewe katika huduma wanazotoa wahusishe suala la uzazi wa mpango ili kama huduma hiyo inatolewa katika vituo binafsi, waweze kufanya maamuzi ya kwenda kutumia huduma anapotaka,

"Pia itaweza kusaidia kuongeza usiri, kwa mtu ambaye anataka huduma hiyo,anaweza kuipata sehemu yoyote bila kukaa foleni,kwa hiyo unajua mimi ninatumia huduma fulani unaenda kwenye duka la dawa kupata huduma, hivyo kama mwingine anatumia kitanzi badala ya kwenda kliniki na kuambiwa kuwa havipo, ataweza kwenda kununua na kuja kuwekewa katika kituo cha afya.

"Pia itatoa nafasi kwa watumiaji wa huduma ya uzazi wa mpango mfano wanaume kupata nafasi ya kukaa na wahudumu kupata ushauri kabla ya kufanya maamuzi,"amesema.

Dkt.Maendaenda amesema kuwa, pia elimu kuhusu huduma za uzazi wa mpango iendelee kutolewa katika maeneo yote nchini ili kupunguza changamoto kwa baadhi ya makundi hususani vijana.
Amebainisha kuwa, sasa huduma za uzazi wa mpango ni bure na zinatolewa na Serikali, lakini wakati mwingine bajeti ya Serikali inakuwa haitoshelezi soko la wahitaji.

Ni zipi njia za uzazi wa mpango?

Tafiti zinaonesha kuwa, kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kutumiwa na mtu au wenza waweze kusubiri,kuchelewesha au kupunguza idadi ya watoto watakaowazaa. Miongoni mwa njia hizo kuna njia za muda mfupi, muda mrefu na za kudumu.

Muda mfupi

Hizi ni njia za kisasa za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuzibadilisha, unaweza kupata ujauzito pindi utakapoacha kuzitumia. 

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa, njia hizi ni nzuri kwa mama anayetaka kupata ujauzito baada ya miaka miwili baada ya kujifungua. 

Miongoni mwa njia hizo ni vichecheo ambavyo ni sawa na vichocheo vya kawaida
vilivyomo kwenye mwili wa mwanamke, njia ya vidonge ambavyo hutumiwa na wanawake kila siku.

Njia ya nyingine ni ya sindano ambapo mama huchoma sindano kila baada ya miezi mitatu,njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango ambavyo huwa vinamezwa na mama ili kuzuia kupata mimba kwa mama anayeshiriki tendo la ndoa au ngono bila kutumia kinga yeyote. 

Hivi vinaweza kuzuia mimba hadi siku tano baada ya kujamiana, kondomu za kike na kiume nazo ni muhimu kutumia ipasavyo kila unapofanya tendo la ndoa au ngono. Hii ni njia ya pekee ambayo pia inazuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa.

Njia za asili

Kukosa hedhi kwa kunyonyesha mfululizo, hii ni njia ya asili ambayo inatokea kwa mwanamke anayenyonyesha na ni ya kuaminika zaidi wakati mama huyo bado hajaanza kuona siku zake za hedhi na ili hayo yote yatokee ni lazima mama awe anamnyonyesha mtoto wake mara kwa mara usiku na mchana na mtoto awe na umri chini ya miezi sita.

Elimu 

Njia hii inawezekana ikiwa mama anaufahamu mzunguko mzima wa siku zake za hedhi na kujua ni zipi siku za hatari za kushika mimba. 

Mama na mwenza wake wanatakiwa kuacha kabisa kufanya tendo la ndoa au ngono siku hizo za hatari.

Kukojoa nje

Njia hii huwa inafanywa na mwanaume wakati wa tendo la ndoa au akishiriki ngono ambapo humwaga shahawa zake nje ya uke.

Njia za muda mrefu

Hizi ni njia ambazo pia zinaweza kurudiwa. Unaweza kupata ujauzito mara utakapoacha kuzitumia. Hizi ni nzuri ikiwa unataka kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine.

Njia ya vipandikizi

Hiki ni kijiti cha plastiki anachowekewa mwanamke chini ya ngozi kwenye mkono wake na kinaweza kuwa kimoja au viwili. 

Hivi huzuia mwanamke asipate ujauzito kwa muda kati ya miaka mitatu hadi mitano kutegemea na aina ya vipandikizi alivyotumia.

Njia ya kitanzi

Ni kifaa kidogo chenye shaba na plastiki ambacho huwekwa kwenye mji wa mimba. Hichi hukuzuia usipate mimba mpaka miaka 12, unaweza kukitoa wakati wowote utakapoamua au kuhitajia kupata mtoto.

Njia ya kudumu

Hizi ni njia huwezi kuzirudia na ukitumia huwezi kupata mtoto tena. Na hutumiwa na watu ambao hawataki kupata mtoto tena. 

Nazo ni kufunga kizazi kwa mwanaume ambapo njia hii inahusisha upasuaji mdogo ambapo mirija ya uzazi ya mwanaume ukatwa au kufungwa hivyo kuzuia yai kusafiri na kukutana na shahawa. 

Mwanaume anaendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kutoa mbegu, lakini mbegu zake hazitaweza kutunga mimba.

Kufunga kizazi kwa mwanamke

Njia hii inahusisha upasuaji mdogo inafanyika kwa kuziba au kukata mirija ya kizazi kuzuia yai kukutana na mbegu, mwanamke ataendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kuona siku zake za hedhi.

Utafahamu vipi kuwa njia gani ya uzazi wa mpango ni sahihi kwako?

Wataalamu wa afya wanasema, inategemea na mtu mwenyewe au wenza kuamua njia gani ni sahihi kwao. 
 
Unashauriwa kutembelea kituo cha afya kilichopo karibu nawe uonane na wahudumu wa afya na wataweza kukufahamisha njia sahihi kwako kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news