Viongozi 52 wamkasirisha Rais Dkt.Mwinyi, atoa maelezo kwa Tume ya Maadili

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Tume ya Maadili ya viongozi wa Umma kujiridhisha ili kubaini sababu za msingi za Viongozi 52 kushindwa kurejesha Fomu za Tamko la Rasilimali na madeni kwa wakati uliowekwa na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria.

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakili, Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amesema, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 jumla ya viongozi 2578 walichukua Fomu za tamko la Rasilimali na madeni ambapo viongozi 2526 walirejesha fomu hizo kwa wakati muafaka, huku viongozi 52 wakirejesha fomu hizo nje ya muda uliowekwa.
Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma Zanzibar wakiwa katika mkutano wa Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. (Picha zote na Ikulu).

Amesema, viongozi waliorejesha fomu hizo nje ya wakati uliowekwa ni namna ya viongozi wanaopewa kazi na kuacha kuzifanya na pale inapotokea wakafanya hukamilisha kwa wakati wanaopenda wao wenyewe.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe.Khamis Ramadhan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Katiba,Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman, wakifuatilia Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Zanzibar, wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akihutubia katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amewakumbusha viongozi wote wa umma waliotajwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuhakikisha wanarejesha Fomu hizo baada ya kuzijaza sio zaidi ya tarehe 31 Disemba, 2021.

Akigusia tatizo la baadhi ya viongozi katika kujaza fomu hizo eneo linalohusu mapato ya biashara, Dkt. Mwinyi amesema fomu mpya iliyofanyiwa marekebisho ambayo itatumika mwaka huu imezingatia suala hilo, hivyo akawataka viongozi kuijaza vizuri ikiwa na taarifa zote muhimu zinazohitajika.
Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akihutubia katika Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Ametumia fursa hiyo kuipongeza Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuwa na ushirikiano na vyombo mbalimbali vya habari na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi na majukumu ya tume hiyo na namna bora ya kuwasilisha malalamiko yao na akabainisha kuwepo wananchi wengi wnaotumia taasisi hiyo kwa lengo la kuimarisha utawala bora.

Ameutaka uongozi wa taasisi hiyo kuendelea kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, udhalilishaji, mgongano wa kimaslahi na tuhuma za rushwa na wizi pamoja na vitendo visivyoridhisha katika jamii,nae akaahidi kuzizfanyia kazi kwa haraka.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewataka viongozi wote waliowateuwa kuwa na utaratibu wa kumpa taarifa za mara kwa mara juu ya hatua walizozichukua dhidi ya watendaji waliobainika kuhusika na ubadhirifu katika taasisi zao, sambamba akatumia fursa hiyo kuipongeza ZAECA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake vizuri.

Amesema,taarifa zinabainisha katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Januari hadi Novemba, 2021 kumekuwepo tuhuma 289 zinazohusiana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ambazo zimechunguzwa.

”Hata hivyo nawataka kuongeza kasi ya uchunguzi, kwani taarifa zinaeleza ni majalada 29 pekee ndio yaliowasishwa Ofisi ya DPP,” amesema.

Amesema katika kuzuia wizi na ubadhirifu wa fedha za umma, Serikali imeweka mkazo katika kufanya ukaguzi wa fedha za Serikali na akabainisha uwepo wa baadhi ya Viongozi wanaochelewesha au kukwamisha matumizi ya mifumo mipya ya malipo na ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletroniki.

Aidha, alieleza kuwepo kwa baadhi ya viongozi wanaokwepa kushirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali kwa kushindwa kutoa taarifa muhimu za ukaguzi na kutaka viongozi hao wafichuliwe na kuchukuliwa hatua.

Raisi Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kushirikiana katika kujenga maadili na kusema panapo maadili haki na uwajibikaji hutawala katika ngazi tofauti.

Rais Dkt. Mwinyi amesema ni vyema kwa viongozi kuitumia siku hiyo kwa kujitathmini na kujipima viwango vya uadilifu na uwajibikaji, uzalendo na utii wa sheria, maadili ya kazi pamoja na madaraka waliyokabidhiwa, sambamba na kutathmini uhusiano wao na mwelekeo wao katika jamii.

Amesema amevutiwa sana na kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Piga vita rushwa, heshimu haki za binadamu, uadilifu na Uwajibikaji kwa maendeleo ya Uchumi endelevu’ kwa kigezo kuwa ni ufupisho wa mambo yote ya msingi yanayohitajika katika kuimarisha maendeleo, kudumisha amani, umoja na mshikamano pamoja na ustawi wa kila mwananchi.

Amesema,utekelezaji wa Utawala Bora bora unahitaji nguzu za pamoja za sekta na wadau wote.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe.Haroun Ali Suleiman akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmin Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kuhutubia hafla hiyo ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa.

Nae, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amewataka wateule wote wa Rais kufuata mwenendo wa kiutendaji wa Kiongozi huyo pamoja na kumsaidia kikamilifu ili kufanikisha azma ya kuijenga Zanzibar kwa kuzingatia uzalendo, uwajibikaji na uadilifu.

Waziri Haroun alitumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Jaji Mkuu Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla kwa kuanza kuifanyia mabadiliko chanya Idara ya Mahakama katika kipindi kifupi tangu ashike dhamana hiyo, sambamba na kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi Talib Haji kwa juhudi mbalimbali anazochukua katika utelezaji wa majukumu yake.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar Ndg.Assa Ahmad Rashid akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Mapema Mwenyekiti, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Asaa Ahmada Rashid alisema Kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Piga Vita rushwa, heshimu haki za binadamu, Uadilifu na Uwajibikaji kwa Maendeleo ya Uchumi Endelevu”inabainisha namna viongozi wa umma na wananchi wanavyopaswa kuwa ili kupata maendeleo ya kweli ya kiuchumi.

Amesema, katika kuimarisha taasisi zilizomo kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali zinazoongoza taasisi hilo ili ziweze kutekeleza vyema majukumu yake.
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Mawaziri wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Alieleza kuwa mapambano dhidi ya rushwa, unyanyasaji na uhujumu uchumi, yataweza kufanikiwa pale patapokuwepo mashirikiano ya pamoja kati ya taasisi hizo na wananchi kwa kuzingatia kuwa wajibu wa kusimamia mapambano hayo hauko kwa taasisi hizo pekee.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news