NA MWANDISHI MAALUM
JAMII ya Wairaqw waishio Dar es Salaam (UMBLUCHA) wamefanya tamasha kubwa Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha jamii ya kabila hilo wanaoishi mijini hawaachi mila na desturi zao, kuwarithisha watoto hasa wanaozaliwa na kuishi mijini, pamoja na kuibua mawazo ya Utalii wa mazao ya Utamaduni.
Bw.Reginald Malley kulia akielekezwa na mzee wa mila kutoka Manyara namna ya kucheza bao la asili ya kabila la Wairaqw kwenye Tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam.
Akizungumza na wanajumuhia ya kabila hilo Mgeni rasmi katika tamasha hilo, Mhe. Balozi Dkt. Willibrod Slaa amewaasa watanzania hasa wazazi kuhakikisha wanaurithisha urithi wa utamaduni kwa kizazi kipya, kwani kwa kupitia urithi huo muhimu watoto wataendela kukua katika maadali mema.
Mzee wa Mila wa Kabila la Wairaqw, Mzee Amatli Buxu akitoa maelekezo ya kimila kuhusu namna kinywaji cha asili ya kabila hilo aina ya Mangure kinavyopaswa kutayarishwa kabla ya kugaiwa kwa watu.
Dkt.Slaa amempongeza Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwenye uhifadhi wa utamaduni wa matanzania hasa kwa serikali anayoingoza kuhakikisha imetenga hela kwa ajili ya kuboresha Kijiji cha Makumbusho kilichopo chini ya Makumbusho ya Taifa nchini.
Mhe. Balozi Dkt. Wilbad Slaa akizungumza na Jamii ya Wairaqw waishio Dar es Salaama na waliotoka Mkoa wa Manyara kwenye Tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini, Dkt.Noel Lwoga, Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Bw. Mawazo Ramadhani Jamvi amesema, taasisi hiyo imejiwekea utaratibu wa kushirikiana na makabila mbalimbali katika kufanya matamasha ya kiutamaduni yenye lengo la uhifadhi na urithishaji wa urithi wa utamaduni.
Licha ya kuwapongeza Jumuiya ya Wairaq waishio Dar es Salaam kwa kuamua kuratibu tamasha hilo, Bw. Jamvi amewahakikishia kuwa Makumbusho ya Taifa itaendela kuwa karibu nao na hata kuhakikisha ujenzi wa nyumba ya kabila hilo unafanyika kwenye kijiji hicho ili kuutangaza na kuhifadhi urithi wa kabila hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho,Be. Jamvi akizungumza na Jamii ya Wairaqw waishio Dar es Salaam na waliotoka Manyara kwenye Tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam.
Dkt.Leonia Hambati ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema yeye amejisikia fahari kuendelea kudumisha utamaduni wake awapo mjini na anafanya hivyo kwa watoto wake bila kuangalia elimu yake wala mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayochochoa kasi ya utandawazi ambao unaharibu mitazamo ya vijana kuhusu utamaduni wao.
Akiongea kwa niaba ya Jamii ya Wairaqw (UMBLUCHA) waishio Dar es Salaam, Dkt.Baltazary Awe amefafanua kuwa, jumuya yao imeona umuhimu wa kufanya tamasha hilo ili kujikumbushia mambo yanayohusu Utamaduni wao, kuhakikisha watoto wao wanajifunza kutoka kwa wazee waishio vijijini, na kuowaonesha wengine utajiri uliopo kwenye utamaduni huo.
Mwenyekiti wa Jamii ya Wairaqw, Dkt.Baltazary Awe akishiriki kikamilifu kwenye Tamasha hilo kwa kuburudika na kinywaji aina Magure kwenye Tamasha la kabila hilo lililofanyika Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam.
Tamasha hilo lililochukuwa siku mbili na kufurahiwa na wageni wa ndani na nje ya nchi, lilipambwa vyema na Ngoma za asili za kabila hilo, vyakula vya asili, majigambo, masimulizi ya wazee nyakati za usiku, mapishi ya pombw maarufu ya kabila hilo ijulikanayo kama Magure, Michezo ya Jadi, dua kutoka kwa wazee wa mila walioombea nchi, Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya Tanzania pamoja na Muungano.