NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua “Ajira Portal Mobile App” itakayotumiwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuendesha mchakato wa ajira Serikalini ambao utaondoa vitendo vya rushwa na upendeleo kwa waombaji wa ajira.
Akizindua programu hiyo Novemba 19,2021 jijini Dodoma, Mhe. Mchengerwa amesema portal hiyo itasaidia kuwapata watumishi wenye sifa stahiki na wazalendo watakaolitumikia taifa kwa weledi, uadilifu na wataolifikisha taifa kwenye uchumi wa kati wa juu.
Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huo wa maombi ya kazi kupitia simu ya kiganjani umelenga kuwapunguzia adha mbalimbali walizokuwa wakikutana nazo waombaji wa fursa za ajira ikiwemo upatikanaji wa taarifa zinazohusu ajira serikalini na mchakato wake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watendaji wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma pamoja na Wadau wa Ajira wakati akizindua Ajira Portal Mobile App jijini Dodoma.
“Mfumo huu ukitumika vizuri, ninaamini waombaji wa ajira wataweza kufanya maombi ya ajira popote walipo mijini na vijijini, kwani mfumo unamuarifu muombaji uwepo wa nafasi.
Mhe. Mchengerwa amewahamasisha waombaji wa ajira serikalini kuanza kutumia mfumo huo ambao utapunguza changamoto nyingi walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya uwepo wa mfumo huo. Kwa kina zaidi tazama video hapa chini;