NA NTEGHENJWA HOSSEAH,OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amewalekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha asilimia 40 na 60 kutoka katika fedha za mapato ya ndani zinazoelekezwa kwenye maendeleo zitekeleze miradi yenye tija.
Waziri Ummy ameyasema hayo alipokua ziarani kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kukagua miradi ya maendeleo na kukutana na Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo.
Akiwa Uyui amesema utekelezaji wa miradi inayotokana na mapato katika maeneo mengi mara nyingi imetekeleza miradi midogo midogo ambayo haileti tija kwa haraka kwa wananchi.
"Unakuta fedha zinapelekwa kidogo kidogo kwenye kila kata, kiasi ambacho hakiwezi hata kukamilisha mradi mmoja mwisho wa siku miradi inabaki viporo kwa muda mrefu mpaka inaharibika na haileti faida kwa wananchi ninachotaka kuona ni fedha hizo zikitumika kwenye miradi yenye mikubwa inayoleta matokeo ya haraka,"amesema Waziri.
"Nataka kuona fedha hizo zinaanza ujenzi na kukamilisha kabisa au zinakamilisha ujenzi wa majengo yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ili yaanze kutoa huduma.
"Tusitake kila kata fedha kidogo mwisho wa siku hakuna matokeo ya fedha mlizoweka,cha msingi mkubaliane maeneo ya kimkakati mjenge miradi ikamilike na ianze kutoa huduma,"amesema.