Yaliyojiri leo Desemba 13, 2021 kwenye hafla ya utiaji saini mikataba baina ya Serikali na kampuni za uchimbaji madini

NA WAANDISHI MAALUM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Madini kusimamia kikamilifu suala la uongezaji wa thamani ya madini yanayozalishwa nchini huku akibainisha kuwa suala hilo haliepukiki.
Mheshimiwa Rais ameyasema hayo katika hafla ya utiaji saini mikataba baina ya Serikali na kampuni za uchimbaji madini iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention Centre-JNICC) jijini Dar es Saalaam.

Rais Samia amesema kama nchi ikifanikiwa kuongeza thamani ya madini fedha nyingi zitabaki nchini na watu watapata ajira.
>Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia safari ndefu ya majadiliano na leo tumeweza kusaini mikataba minne hapa.
>Namshukuru pia Waziri na Viongozi wote wa Wizara ya Madini kwa kunialika kuja kushuhudia jambo hili kubwa na la kihistoria katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu

>Kipindi cha nyuma tulisikia tu kwamba makampuni yanachimba madini kwenye nchi yetu, tena tulisikia kwenye sauti za Wananchi mara nyingi wanapopiga kelele kuhusu uharibifu wa mazingira na uharibifu wa vyanzo vya maji, lakini hatukujua kinachofanyika huko, wala kinachochimbwa na kinakwenda wapi, lakini leo hii tunashiriki kama wabia muhimu wa uchimbaji wa rasilimali zetu hizi muhimu na adhimu ambazo zina nafasi ya kipekee katika kuiletea nchi yetu maendeleo ya kiuchumi, hatuna budi kujipongeza kwa hatua hii tuliyofikia
>Ndugu zangu kila safari huanza na hatua moja, na hatua ya safari hii sikuanza mimi, alianza Mwenzetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye Mungu alimpa ujasiri akasema HAPANA, rasilimali zetu sasa imefika wakati zifaidishe Nchi na Wananchi kwa ujumla, nae ndio alianza hatua ya kwanza, kwa hiyo niombe kila mmoja wetu amuombee kwa Mwenyezi Mungu ailaze Roho yake Mahali Pema Peponi.

>Watoto wetu wa Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma wameimba Rais ameuwasha Moto na hauzimiki, lakini kwa moto wa madini aliyeuwasha alikuwa ni Dkt.John Pombe Magufuli, nami naahidi hautazimika na nitakwenda nao.

>Kama mnavyofahamu kuwa Nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali mengi tu ikiwepo Dhahabu, Chuma, Nickel, Fedha, Shaba, Tanzanite na mengineyo na leo nimesikia kuwa mchanga wa Pwani nao una madini yana kazi ya kufanya, tumshukuru Mungu kwa kutubariki na mambo yote haya.
>Lakini kubarikiwa na Madini haya ni jambo moja na kuyachimba kwa manufaa ya Watanzania ni jambo lingine, ili kuhakikisha wenye rasilimali hizi ambao ni wananchi wananufaika nazo, Serikali iliamua kufanya mabadiliko makubwa ya sheria zinazosimamia sekta hii ya Madini ili kuipa nguvu Serikali kumiliki rasilimali hizi kwa niaba ya wananchi na kwa maslahi mapana ya Taifa.

>Makubaliano tunayoyashuhudia leo kati ya Serikali na Kampuni hizi za uchimbaji wa madini ni matokeo ya jitihada hizo, lengo ni kuiwezesha Serikali kuwa na ubia chini ya kampuni moja itakayowezesha shughuli za uchimbaji wa madini kama mbia baina ya Mwekezaji na Serikali, kampuni hizo za ubia ndizo zitakazosimamia uchimbaji kwenye maeneo mbalimbali tuliyotoa leseni za uchimbaji ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanasimamiwa ipasavyo.
>Azma ya Serikali ni kuona kuwa Taifa letu linanufaika ipasavyo na rasilimali ya Madini, pamoja na kuona Wawekezaji wanapata manufaa kutokana na uwekezaji wao, kupitia miradi hii, Serikali itapata manufaa mbalimbali ikiwepo Kodi, Tozo, Ajira, gawio lakini pia uuzaji wa huduma ambazo makampuni watakuwa wanafanya wafanyabiashara ndogo ndogo wa nchini pamoja na kurudisha hisani kwenye maeneo ya miradi hii ambayo ipo.

>Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na uchakataji wa madini zinazimamiwa vizuri ili tuweze kunufaika na madini yetu zaidi.

>Rai yangu kwa Wizara ni kuendelea kusimamia kikamilifu suala la uongezaji wa thamani wa madini yetu ambalo haliepukiki, kuna kampuni ambayo leo ilikuwa isaini hapa, lakini baadaye tena wakakataa tena kipengele hiki cha kuweka thamani ya madini hapa nchini na ndio maana leo wamechelewa kusaini hapa.
>Lakini nirudie kwamba tutachimba, tutachenjua, tutafanya kila kitu na kuongeza thamani ya madini yetu hapa nchini.

>Tukifanikiwa kongeza thamani madini yetu ni dhahiri kuwa fedha nyingi itabaki hapa nchini na Vijana wetu watapata ajira, lakini pia mwekezaji ambaye anataka kuchimba aende na mnyororo wa thamani ya madini yetu, tunawakaribisha waje, tutafanya nao kazi, lakini wajue kwamba ubia utakwenda mpaka kwenye kuongeza thamani ya madini.

>Lengo letu ifikapo mwaka 2025 Sekta hii ya Madini iweze kuchangia kwa asilimia 10 ya pato la Taifa na kwa mwendo huu tunaokwenda nao sina shaka tunaweza kufika hapo au tukazidi kidogo lakini nina uhakika kwa sababu sasa tupo kwenye asilimia 6.7 tunaweza kufika asilimia 10 baada ya miradi yote hii kuanza na kutekeleza kazi zao.
>Nimefurahi kusikia wawekezaji hawa kila mmoja aliyezungumza amelijua suala la uongezaji thamani hapa nchini, kwamba tunawapa leseni tumeingia nao ubia lengo ni kuongeza uchumi wa nchi hii, lengo ni kuleta maslahi mapana ya Taifa hili, nimefurahi kusikia kutoka midomoni mwao.

>Ili kuhakikisha nchi yetu inapata faida katika Sekta ya Madini Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa madini katika maeneo yote ya uzalishaji, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka za ulinzi na usalama zimeendelea kuhakikisha kuwa katika maeneo ya Viwanja vya Ndege, Bandari na Mipakani kunakuwa na usimamizi madhubuti ili kuzuia utoroshaji wa madini na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinakuwa na manufaa kwa Watanzania.

>Huwa tunasikia yanapenya huku mara kule, jitidada zinafanywa kuzuia utoroshaji wa madini, niwaombe waliopewa dhamana ya kusimamia utoroshaji wa madini wajitahidi kudhibiti.

Aliyoyasema Waziri wa Madini, Dotto Biteko

>Sekta hii ya Madini Mheshimiwa Rais umeipa msukumo mkubwa sana, tupo hapa leo kwa sababu ya msukomo wako, kwenye historia ya sekta ya Madini leo tunasimama kifua mbele kwa sabau historia inakwenda kuandikwa, kwamba mikataba mikubwa minne inasainiwa na ambayo thamani yake ni Mabilioni ya fedha, Jumla ya Dola za kimarekani 763 zinakwenda kuwekezwa kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sawa na Trilioni moja na milioni miasaba na hamsini, uwekezaji huu mheshimiwa Rais umetokea wewe ukiwa ni Rais wetu.
>Mheshimiwa Rais Sekta hii imekua, makusanyo baada ya wewe kuingia kwenye ofisi yameongezeka sana, tulikuwa tunakusanya mauzo yote ya dhahabu nchi nzima ni Shilingi Trilioni 8.19, lakini kwa miezi sita peke yake toka umekuja tumeshafanya mauzo ya madini ya Trilioni 4., hii haitupi wasiwasi kiasi kwamba lengo tulilowekewa la kukusanya shilingi Bilioni 6 kwa mwaka kutoka Bilioni 580 tuliyokuwa tumepangiwa tutalivuka kwa sababu umeweka msukumo mkubwa sana kwenye miradi hii ya maendeleo.

>Kingine kinachotupa ujasiri pamoja na kwamba ni muda mfupi umeingia ofisini ziara ulizofanya za kuwaita wawekezaji, wamesikia wito wako, wamekuja kwa wingi sana, kwa kipindi kifupi tumeshatoa leseni za uchimbaji madini 20, 277 za wachimbaji wakubwa, wakati na wadogo.
>Nafurahi kusema wawekezaji wengi wanaofanya tafiti za madini kwenye maeneo mbalimbali wamekuja kwa wingi na tayari tumeshatoa leseni 476 za kampuni za utafiti wa madini, mambo yanayofanywa ni mengi.

>Naomba niwatoe wasiwasi wananchi wote wa Tanzania popote mlipo ambapo miradi hii inakwenda, leo tumesaini mikataba hii na leseni tumezitoa hatua inayofuata ni kazi ya uchimbaji madini, lakini kabla ya kuchimba ni lazima watanzania wote popote mlipo kwenye maeneo haya ni lazima mlipwe stahiki zenu, Mheshimiwa Rais alishatuelekeza, hakuna hata milimita moja ya Mtanzania itakayoondolewa bila mtanzania huyo kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

Aliyoyasema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala]

>Tunayo furaha kubwa ya kuwa mwenyeji wa tukio hili la utiaji saini mikataba ya uchimbaji madini, niwakaribishe wote katika mkoa huu, Mkoa wetu ni Salama na tunaendelea kuupendezesha

>Mkoa wa Dar es Salaam tulikutana na wachimbaji wa madini wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam na Wanunuzi wa Madini na niliwatembelea katika soko lao la madini hapa Dar es salaam.
>Wachimbaji na wadau wa Madini walinipa salamu za pongezi za uamuzi wako wa uanzishaji wa masoko ya madini kwa sababu imeongeza uwazi wa masuala ya madini,kwamba watu wanakutana wapi muuzaji na mnunuzi.

>Tuliona soko lao na wamekiri kwamba mapato ya Serikali yameongezeka na wao wanaona fahari kuchangia pato la Taifa kwa maana ya Kodi

>Wamesema kwa uanzishaji wa masoko haya umeweza kudhibiti utapeli wa madini, na kwa hapa Dar es Salaam Watu walikuwa wanalizwa sana, badala ya kuuziwa madini wanauziwa chupa.
>Kwa sababu Makao Makuu ya Nchi yapo Dodoma, Dar es Salaam unabaki kuwa mkoa mkubwa wa kibiashara, maombi yao ni soko kubwa la madini liwe hapa Dar es Salaam, yaani iwe kama Dubai, nami niliwakubalia ndio maana unaona kuna safisha safisha, pendezesha Dar es Salaam na Mheshimiwa Lukuvi atanikabidhi master plan ya Dar es Salaam.

Imeandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news