NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 71 wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni kwa ajili ya kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya Mheshimiwa Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo hivi karibuni.
Katibu Msaidizi mkuu Idara ya Oganazesheni CCM, Solomon Itunda, akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 15,2022 jijini Dodoma amesema kuwa, idadi ya wanachama waliochukua fomu katika siku ya mwisho wa zoezi hilo imefika 71.
Itunda amesema kuwa, kwa jana jumla ya wanachama watano walichukua fomu na kufanya idadi kufikia wanachama 71 baada ya wale 66, waliokuwa wamechukua hadi juzi.
“Leo hii tumepokea wanachama watano ambao wamejitokeza katika vituo vyetu vya Dodoma na Dar es Salaam kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hii ya Uspika iliyoachwa wazi,"amesema.
Pia amesema, katika kituo cha Dodoma mwanachama mmoja ndiye aliyejitokeza kuchukua fomu wakati katika ofisi ya Lumumba ni wanachama wanne na ofisi kuu ya Zanzibari hakuma aliyechukua.
Itunda amemtaja aliyechukua fomu ofisi kuu Dodoma kuwa ni Samwel Magero.
“Ofisi ndogo ya Lumumba waliochukua fomu ni Rahimuddin Ismail, Alex Mwita,Themistocles Laurian Rwegasira pamoja na Grangay Nyalohala,”amesema.
Amesema kuwa kukamilika kwa zoezi hilo la kuchukua fomu lililoanza Januari 10 mwaka huu kunatoa nafasi kwa vikao vingine kuanza.