Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kiteto afunguka kuhusu uraia wake Tanzania

NA MOHAMMED HAMAD

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mheshimiwa Emmanuel Papian kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amevunja ukimya na kueleza namna yeye na wazazi wake walivyoweza kuingia nchini Tanzania wakiwa wanakimbia vita wakitokea nchi ya Rwanda.
Mheshimiwa Papian ameyasema hayo jijini Dodoma kwenye maziko ya marehemu baba yake, Mzee Papian John aliyefariki Januari 1, 2022 akiwa na tatizo la sukari na kuzikwa Dodoma na mamia ya wananchi wakiwemo wa Kiteto kushiriki katika safari ya mwisho ya baba yake hapa duniani.

Amesema, yupo nchini kisheria, wala hana makandokando ambayo yanaweza kumfanya aondolewe nchini na kuwataka wanaomchafua kwa maslahi binafsi waache kwani yupo kisheria.

Amesema akiwa Kiteto aliwaacha wazazi wake Karagwe na aliwahi kufanya kazi mbalimbali za chama na Serikali aliwahi kuwa Ofisa Kilimo na Mifugo Kata ya Dosidosi na baadaye alichaguliwa kuwa MNEC na pia alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kiteto na kuongoza kwa miaka mitano.

"Marehemu Baba yangu alikimbilia Tanzania wakati wa vita baadaye aliomba uraia kisheria na kupata rasmi mwaka 1980 akiwa na mama yake pamoja na ndugu zao wakitokea Rwanda, ambapo waliishi Karagwe na baadaye Bukoba Tanzania,"amesema.

Amesema, kwa kuwa marehemu baba yake alikuwa na ujuzi wa ufundi wa viatu aliweza kutumiwa kama fundi mkuu wa kiwanda cha viatu cha ngozi na mikomba ya wanawake mwaka 1983.

Mheshimiwa Papian amesema,uhusiano wake na wananchi hasa wa Kiteto ni wa miaka mingi toka alipofika mpaka alipoweza kuwa mwakilishi wa wananchi nafasi ya Ubunge wa jimbo hilo la Kiteto.

"Kuna vijimaneno humu mtu anasena Papian sio raia, Emmanuel sio raia na mara nyingine tunatukanwa na watoto ambao tumewazaa...mimi nina miaka 28 Kiteto, sasa wale watoto ambao mama zao wako hapa na baba zao na babu zao mimi nimeishi nao...

"Nimekula nao kwenye nyumba zao, nimekwenda nao hospitali ili hao watoto wazaliwe, nimewabeba kwenye magari yangu nilipopata kauwezo, tulikoroga uji nilipokuwa na njaa tukanywa sikuwabagua, tukiishi kama ndugu kwa sababu wale watoto hawana historia wakisikia wanatukana yawezekana kuna wanaowashawishi watukane wee... sema tu kwenye mitandao, lakini madhara yake ni makubwa.
"Kiongozi mzuri au baba mzuri ni yule aliyelelewa na maadili, huwezi kujibu jibu unapotukanwa..leo kuna mtu mmoja anaitwa... aliyedaiwa alikuwa anatukana mitandaoni sasa ameamriwa na Mahakama kumlipa mamilioni ya fedha aliyemtukana.

"Hivi Papian anaanzia wapi, tulijenga misikiti, Makanisa, tumeshirikiana kwenye misiba, masika na kiangazi nimkamate mtoto wa Kiteto nimweke ndani kisa ametumika vibaya na watu kunichafua hivi anaweza kuchomoka kweli.

"Lakini pia sio mimi natukanwa peke yangu kuna viongozi mbalimbali wanatukanwa kuna Marais wanatukanwa ndio maisha hayo, lakini nitumie nafasi hii kusema wazazi na viongozi hebu semeni hili, ili Dunia isipoteze mmomonyoko wa maadili,"amesema Mhe. Emmanuel.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news