NA MWANDISHI DIRAMAKINI
ALIYEKUWA Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dkt. John Mahene amerejea na kutubu kwa uongozi na kanisa la EAGT baada ya kuasi imani ya kanisa hilo toka mwaka 2016.
Aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dkt. John Mahene akipokelewa katika kanisa na Mshauri Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Denis Livingstone (kulia) na kushoto ni Mchungaji Alex Simbila wakati wa mkutano maalum wa kurejea kwake katika kanisa hilo.
Akizungumza mbele ya kikao kilichojumuisha Maaskofu wa ngazi ya Taifa, Kanda na Majimbo ya kanisa hilo mapema Januari 18, 2022 katika Kanisa la EAGT Mlimwa West Jijini Dodoma linaloongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Brown Abel Mwakipesile alieleza msukumo wa hatua yake ya kuomba msamahe kwao ili aendelee kutumika kwa amani na kusema yupo tayari kuachilia mambo yote na kuahidi kurejea katika msingi wa kanisa.
Mchungaji Mahene alieleza kuwa ni kipindi kirefu hakuwa pamoja nao hivyo ameamua kurejea kwa toba huku akiliomba kanisa lote kumsamehe ili aanze upya na kuendelea kumtumikia Mungu.
“Sina neno zaidi ya nisamehewe, nisameheni ni hilo tu na ninaomba kesi zote zinazoendelea zifutwe narudia tena nisameheni,”alisema Mahene.
Aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dkt. John akiomba msamaha mara baada ya kuamua kurudi kwenye imani ya kanisa hilo baada ya kuasi toka 2016. Ameomba msamaha huo Januari 18, 2022 katika mkutano uliojumuisha Maaskofu wa Kanisa kuanzia ngazi ya Taifa, Kanda na Majimbo.Mkutano ulifanyika katika kanisa la EAGT Mlimwa West Dodoma.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Askofu Mkuu wa Kanisa, hilo Dkt. Mwakipesile alieleza kufurahishwa na hatua hiyo huku akisema ni majibu ya maombi ya kanisa kwa kipindi kirefu na kuwatia moyo waumini kuimarika na kuendelea kumtegemea Mungu kwa kuamini hujibu maombi kwa wakati sahihi huku akionesha shukrani kwa Mungu kwa hatua ya kurejea na kutubu kwa mchungaji huyo.
Aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. John Mahene (kushoto) pamoja na Mchungaji wa Kanisa la EAGT Sinai Mchunghaji Christopher Kushoka wakiungana na kanisa kuomba maombi ya shukrani mara baada ya kurejea na kuomba msamaha kanisa la EAGT Jijini Dodoma.
“Kipekee ni siku ya ajabu sana na tunamshukuru Mungu amabaye amesema na ndugu yetu na neema ikamjia amerejea, hivyo niwasihii kanisa tusamehe na tuyasahau yote, tuliomba na Mungu ametenda,” alisema Askofu Mwakipesile.
Pia aliongezea kuwa, Kanisa litaendelea kusimama naye huku likiomba kwa bidii ili kuendeleza kazi ya Mungu waliyoitiwa kila mmoja kwa nafasi yake.
Baadhi ya Maaskofu wa Kanisa la EAGT wakifuatilia mkutano huo.
Aidha Aliwaasa waumini wa kanisa hilo kuendeleaa kusimama imara katika imani na kusema kuwa Mungu ni mwaminifu na hutenda mambo kwa wakati wake huku akiwasihi kudumu katika maombi maana Mungu anaweza mambo yote.
“Mungu awabariki kwa maombi songeni mbele kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu, tumshukuru Mungu kwa pamoja kwa ndugu yetu Mahene maana Mungu ni mwaminifu kwa mamabo magumu yanapotokea na hutoa majibu,”alisema Askofu Mwakipesile.
Askofu wa Jimbo la Temeke, Mchungaji Japhet Mkinga alitoa neno la shukran kwa niaba ya maaskofu wengine na kumpongeza Mchungaji Mahene kwa utayari na kuonesha ujasiri wa hatua hiyo, wakati wa mkutano huo.
Aliongezea kuwa, kanisa limempokea kwa moyo mmoja na kueleza kuwa ni shahuku ya Mungu mtu anapoona kosa na kurejea kwa toba yeye Mungu husamehe.
“Tumempokea ndugu yetu na sisi kama wakristo kuwa na migogoro siyo moyo wa Mungu, hivyo tuzidishe umoja na mshikamano miongoni mwetu na Mungu ambariki kwa maamuzi hayo,”alisisitiza Askofu Mwakipesile.
Katibu Mkuu wa Kanisa EAGT, Dkt.Leonard Mwizarubi akisoma barua iliyoandikwa na aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. John Mahene iliyohusu ombi la kusamehewa na kanisa mara baada ya kuasi imani hiyo toka 2016, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano.
Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT Sinai Christopher Kushoka alieleza historia fupi ya kisa cha kutaka kurejea kwa mchungaji huyo, alisema ni baada ya Mungu kusema na Mchungaji Mahene na kumuonesha maangamizi endapo hatotengeneza na Mungu na kurejea kwenye imani.
“Alisema Mungu alimsemesha mwenyewe kupitia ndoto na kuona ni lazima amuone Askofu Mkuu na kuomba msamaha mbele ya kanisa na kutaka kurudi tena,”alisema mchungaji Kushoka.
Kwa upande wake Makamu Askofu wa Jimbo la Temeke, Japhet Mkinga alitoa neno la shukran kwa niaba ya maaskofu wengine alimpongeza Mchungaji Mahene kwa utayari na kuonesha ujasiri mkubwa wa kurudi kwa unyenyekevu na kuomba msamaha kwa kanisa.
Askofu Mkuu wa Kanisa Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dkt. Brown Abel Mwakipesile akiongoza maombi ya shukran kwa Mungu mara baada ya aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. John Mahene kurejea na kutubu mbele ya viongozi wa kanisa baada ya kuasi imani hiyo.
“Mioyo yetu imejaa furaha sana, tunaujasiri katika Kristo Yesu na ni jambo la baraka, hii imetupa ujasiri, uthabiti na kujisikia tupo sehemu sahihi na tunakushukuru baba yetu kuweza kurudi na kuisimamia kweli ya ndani ya moyo wako kwa kutubu na kurudi tunambariki Mungu kwa haya yaliyotendeka,” alisema Mchungaji Mkinga.
Baadhi ya Maaskofu wa Kanisa la EAGT wakifuatilia mkutano huo.
Kuhusu EAGT
Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) limejikita katika kueneza injili kwa kila kiumbe, ambapo lilisajiliwa rasmi tarehe 18, Julai 1991.
Kanisa limeendelea kuongozwa na Mungu mwaka hadi mwaka na hadi sasa lina washirika wengi walio ndani ya Makanisa na matawi yake zaidi ya 4000 yaliyoenea nchi nzima kwenye Majimbo 81 na Kanda 9 hadi Juni 2019.
Tangu EAGT ilipoanza huduma nchini ilikuwa chini ya uongozi wa Hayati Askofu Dkt.Moses Samwel Kuloka, uongozi wa kanisa umeendelea kujengeka toka Taifa hadi kanisa la Mahali Pamoja (KMP).