NA GODFREY NNKO
MWANASIASA mkongwe nchini, Mheshimiwa Juma Duni Haji (Babu Duni) ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Hayati Maalim Seif Sharrif Hamad ametangazwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo.
Wakati wa uhai wake, Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ndiye alikuwa anaongoza nafasi hiyo.
Babu Duni ameshinda nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho uliofanyika usiku wa kuhamkia leo Januari 30,2022 jijini Dar es Salaam.
Kwa muda nafasi hiyo ilikuwa wazi baada ya kifo cha Maalim Seif Shariff Hamad aliyefariki Februari 17, 2021.
Ushindi huo unatokana na kura 339 alizozipata kati ya kura halali 464 huku Mheshimiwa Othman Masoud Othman akipata kura 125.
Wajumbe katika mkutano walikuwa 470 na kura zilizopigwa zilikuwa 468 ambapo zilizoharibika zilikuwa nne.
Kwa matokeo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar wa Chama cha ACT Wazalendo huku Msafiri Mtemewa akishinda nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu.
Babu Duni
Huyu ni mwanasiasa mkongwe ambaye alizaliwa Novemba 26 mwaka 1950, alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Hayati Maalim Seif Sharrif Hamad.
Kabla ya ushindi huu alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar.
Babu Duni ni kiongozi mwenye uzoefu kwenye siasa za Zanzibar na alikuwa mmoja wa mawaziri waliofanya vizuri ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mwaka 2010-15 akisimamia Sekta ya Afya.
Aidha,Babu Duni ni mwalimu kitaaluma kama alivyokuwa Maalim Seif na alisomea shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kwa shahada ya Umahiri.