NA MWANDISHI DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Gavana wa Benki Kuu ya Uganda, Profesa Emmanuel Tumusiime-Mutebile kilichotokea asubuhi ya leo Januari 23, 2022 jijini Nairobi, Kenya ambapo alikuwa akitibiwa.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 23, 2022 na Benki Kuu ya Tanzania ambayo imefafanua kuwa, inatoa pole kwa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa Benki Kuu ya Uganda, familia yake, wananchi wa Uganda na Jumuiya ya Benki Kuu katika ukanda wetu.
Kwa mujibu wa BoT, Gavana Tumusiime-Mutebile atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa maendeleo ambayo Benki Kuu ya Uganda imepata katika kipindi cha uongozi wake, ikiwa ni pamoja na kuifanya benki hiyo kuwa mbele katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika utendaji kazi wake.
Sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha nafasi ya Benki Kuu katika kufikia mtangamano wa kikanda na ushirikiano wa kiuchumi kupitia Kamati ya Masuala ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza kufuatia taarifa ya kifo hicho, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Florens Luoga amesema kuwa, "Benki Kuu katika kanda yetu zimefaidika sana na mchango mkubwa wa Profesa Tumusiime-Mutebile katika mikutano ya majadiliano ya Kamati ya Masuala ya Kifedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hasa kutokana na uzoefu wake wa kazi. Tutakumbuka uongozi wake,"amefafanua Profesa Luoga.
"Profesa Tumusiime-Mutebile alianza kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Uganda mwaka 2001 hadi mauti ilipomkuta, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,"imeongeza sehemu ya taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania.