Biashara United yasaini kandarasi ya miezi sita na Kocha Mkuu raia wa Burundi

NA FRESHA KINASA

TIMU ya Soka ya Biashara United Mara inayoshiriki Ligi Kuu (NBC Premier League ) imemtambulisha rasmi, Vivier Bahati raia wa Burundi kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo kwa kipindi cha miezi sita. 
Kocha huyo ametambulishwa leo Januari 18, 2022 makao makuu ya timu hiyo yaliyopo Kata ya Mukendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Katibu wa Biashara United Mara, Khaji Mtete amesema kuwa, timu hiyo ilifanya mchakato wa kutafuta kocha mpya baada ya kocha aliyekuwepo Patrick Odhiambo raia wa Kenya kuondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili. 

Mtete amesema kuwa, kocha Vivier mwenye leseni B ya CUF atahudumu kwa kipindi cha miezi sita ambapo timu ikiridhishwa itaingia naye kandarasi ya kipindi kingine kuinoa. Huku akisema kuwa Mwalimu huyo anasifa, uzoefu na uwezo mzuri kuisadia timu hiyo kutoka sehemu ilipo sasa.
"Niwaombe wapenzi na mashabiki wa Biashara United Mara wampe ushirikiano wa dhati aweze kuongoza benchi la ufundi ili timu yetu iweze kufanya vyema zaidi katika michezo yake yote,"amesema Mtete.
Kwa upande wake Kocha Vivier Bahati amesema kuwa, amefurahi timu hiyo kumpa kandarasi hiyo ambapo amesema hali ya timu hiyo si nzuri licha ya kucheza mpira mzuri lakini ameahidi kupambana kuhakikisha timu inakuwa na matokeo mazuri kwani Biashara United aliyozoea kuiona kipindi cha nyuma kwa sasa ni tofauti.
"Tunaomba ushirikiano kwa wana Mara wote wanaoipenda timu, ninaamini Mungu atatufungulia mlango kutokana na nguvu na juhudi zetu kwa pamoja zitaiweka Biashara United kuwa sehemu nzuri," amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news