NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Brigedia Jenerali Gabriel Saul Mhidze amewataka watumishi wa kada ya afya nchini kuwa, wazalendo na kufanya kazi zao kwa weledi, ili kwa Pamoja kuweza kutimiza adhima ya serikali ya kuboresha afya za wananchi, kupitia miradi mbalimbali ya afya inayoanzishwa nchini.
Brigedia Jenerali Mhidze amesema, iwapo kada hiyo ya afya itakubali mabadiliko chanya yanayofanywa na Serikali, kutakuwa na ahueni kubwa kwa wananchi, kwani serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kupunguza gharama za matibabu, kuboresha miundombinu ya afya, sambamba na kusogeza huduma mbalimbali za afya karibu na wananchi, ikiwemo huduma za uchujaji damu kwa wagonjwa wa figo nchini.
Ametoa rai hiyo leo Januari 6,2022 kwenye Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo maalum ya uchujaji sumu kwenye damu kwa wagonjwa wa figo nchini, yaliyotolewa kwa wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, ili kuwajengea uwezo na umahiri katika kutumia mashine mpya na za kisasa zilizonunuliwa na MSD na zinatarajiwa kusambazwa katika hospitali mbalimbali nchini.
“Kumekuwepo na watumishi wenzetu wasio waaminifu na waliokosa uzalendo, ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakitumika kwa nia ovu ya kukwamisha mradi huu mahususi kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, ambao umelenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi sambamba na kuwasogezea huduma hizi za uchujaji damu huko walipo,”amesema Brigedia Jenerali Mhidze.
Pia amewatunuku vyeti wahitimu hao na kuwataka kuwa mabalozi wazuri huko waendako, kwa kueneza mazuri waliyojifunza, ili hospitali zingine ziweze kuhamasika na kuanzisha huduma hizo za kibingwa katika maeneno yao.
“Mimi ni askari ambaye nina wajibu wa kulinda raia na mali zao, hivyo kamwe sitakubali kuona watu wachache wanahujumu juhudi hizi za Serikali, ambazo lengo lake kuu ni kuboresha afya za wananchi, na kuwapunguzia mzigo wa gharama kubwa za huduma hii ya uchujaji damu, hivyo nawasihi wahitamu mkawe mabalozi wema kwa watumishi wenzenu,”amebainisha Brigedia Jenerali Mhidze.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uchujaji Damu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Linda Ezekiel amesema, mafunzo hayo ni endelevu na ofisi yake inaandaa mkakati maalum wa mafunzo, ambao utatumika kuwajengea uwezo watalaamu hao mara kwa mara, hivyo kuwasihi kutumia ujuzi walioupata katika kuboresha huduma za uchujaji damu kwenye vituo vyao vya kazi, ili kuwapunguzia wananchi mzigo.
Dkt. Linda amemshukuru Brigedia Jenerali Mhidze na wadau mbalimbali kwa utayari wao katika kuleta mapinduzi katika matibabu ya kuchuja damu nchini, huku akiushukuru uongozi wa Hospitali ya Jeshi Lugalo chini ya Brigedia Jenerali, Dkt.Fredy Kivamba kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo.
Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi ameelezea uwepo kwa ongezeko kubwa la wagonjwa wenye matatizo ya figo nchini, huku akiwataka wataalamu kufanya kazi zao kwa nidhamu na weledi ili lengo lililokusudiwa na serikali kupitia mafunzo hayo liweze kutimizwa.
Sambamba na hilo amewataka wananchi kubadili mitindo hatarishi ya maisha ikiwa ni pamoja na kupima afya zao mara kwa mara ili kujua yanayowasibu mapema pamoja na kufanya mazoezi.
Naye mwakilishi wa wahitimu hao, Dkt.Pantaleo Joseph ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo adhimu, na kuupongeza uongozi wa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo kwa kuwakarimu wakati wote wa mafunzo hayo, huku wakiomba mafunzo hayo yawe endelevu na yawafikie wenzao walioko katia vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, kwani yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma na kuokoa Maisha ya wananchi.