NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepitisha jina la Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo leo Januri 20, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Ameyasema hayo,baada ya kumalizika kwa kikao maalum kilichoongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Shaka amesema kuwa, kikao hicho kimekaa kwa taratibu na kwa mujibu wa katiba ya CCM ambacho kimejadili mambo mbalimbali ikiwemo majina ya waliowania nafasi ya Spika na kufikia maamuzi ya kumteua Naibu Spika wa Bunge kuwania nafasi hiyo.
“Pamoja na mambo mengine kamati hii ilipitia na kuchambua majina ya walichukua fomu za kuwania nafasi ya uspika na kumteua Naibu spika Tulia Akson kuwania nafasi hiyo ambapo kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi kitakaa Januari 30, mwaka huu na kumpigia kura,”amesema.
Aidha, kamati hiyo imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, katika utendaji wake wa kazi kwa kuhakikisha wanafunzi wote nchini wameingia kidato cha kwanza kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa madarasa huku kikimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi kutokana na utendaji wake kwa kusimamia uchumi wa bluu.
“Chama kimeridhishwa na mabadiliko kupitia uchumi wa bluu, chama kimeridhishwa na mabadiliko hayo kwa hiyo CCM imerdhishwaa kabisa na utendaji wa serikali zote mbili. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Kikao Maalumu cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika leo tarehe 20 Januari, 2022 katika ukumbi wa Halmashauri Kuu CCM White House Jijini Dodoma.
“Chama kimefuatilia kwa ukaribu sana serikali kuhusu ufanyaji kazi wa Serikali na kimejiridhisha na kazi nzuri zinazofanywa na marais wa pande zote mbili Bara na Zanzibar,"amesema Shaka.
Hata hivyo, mchakato wa uchukuaji fomu za kuwania nafasi ya Spika ulianza Januari 10, mwaka huu na kumalizika Januari 15, mwaka huu huku waliochukuwa fomu wakifikia 71 na waliorudisha walikuwa ni 70, kufuatia aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo Januari 6, 2022.