NA GODFREY NNKO
STRIKA wa Al-Nassr Football Club ya nchini Saudia Arabia ambaye pia ni naodha wa timu ya Taifa ya Cameroon, Vincent Aboubakar ameiwezesha timu yake kuanza vema katika michuano ya AFCON 2022 nchini Cameroon.
Picha na AFP via Getty Images.
Aboubakar amefunga mabao mawili, yote yakiwa ni ya penalti dhidi ya Burkina Faso katika mchezo wa Kundi A.
Mabao ya Aboubakar yalipatikana katika dakika ya 40 na lingine dakika tatu za majeraha baada ya 45 za kwanza.
Katika mtanange huo wa ufunguzi wa Mashindano ya Ubingwa barani Afrika (AFCON 2022) uliopigwa The Paul Biya Stadium (Olembe) mjini Yaounde, wenyeji hao dakika tisini ziliisha kwa kujizolea alama tatu kwa mabao 2-1.
Awali,Gustavo Sangare katika dakika ya 24 aliwanyanyua mashabiki wa Burkina Faso kwa bao la kwanza ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo ulikuwa zawadi tosha kwa Rais wa Cameroon, Mheshimiwa Paul Biya ambaye alikuwa uwanjani hapo kushuhudia kazi ya vijana wake katika mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Katika mechi nyingine ambayo imepigwa katika dimba hilo Januari 9,2022 timu ya Taifa Cape Verde imejizolea alama tatu kwa kuwachapa Ethiopia 1-0.
Mambo yaliwaendea ovyo timu ya Taifa ya Ethiopia baada ya mchezaji wao Yared Bayeh Belay kupewa kadi nyekundu dakika ya 12 ya kipindi cha kwanza.
Licha ya kuwa pungufu waliendelea kutandaza kabumbu safi ingawa kabla ya kipindi cha kwanza kufikia tamati, Cape Verde walianza kuburudika. Ni dakika ya 45 na ushee ambapo, Strika Julio Tavares aliachia mkuki wa moto.
Bao hilo lilidumu hadi mwisho wa mchezo ambapo ubao ulisoma Cape Verde 1-0 dhidi ya Ethiopia.
Leo Januari 10,2022 michezo minne itachezwa kama inavyoonekana hapa chini;