NA FRESHA KINASA
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Mkoa wa Mara umepokea msaada wa vyakula ikiwemo mchele kilo 100, maharage kilo 100, pamoja na fedha kiasi cha shilingi 500,000 kutoka kwa Mgodi wa CATA MINING uliopo eneo la Kataryo Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Ambapo msaada huo utakabidhiwa Februari 3, 2022 na UWT katika Kituo cha Nyumba Salama kinachotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania katika kuadhimisha miaka 45 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi.
Ambapo maadhimisho hayo kitaifa yatafanyikia katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
"Niushukuru Mgodi wa CATA MINING tuliandika barua ya kuomba kusaidiwa ili na sisi tuwasaidie Watoto wenye uhitaji na wao bila kusita wametoa msaada huu. Kama jumuiya ya tutapeleka msaada huu kwa watoto wenye uhitaji, waliokimbia ukatili wa kijinsia katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Butiama katika kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama chetu cha mapinduzi,"amesema Hassan.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema kuwa jamii inawajibu wa kuendelea kuwajali watoto wenye uhitaji katika jamii pamoja na makundi mengine kwa kuonesha upendo wa hali na mali ili kuzidi kujenga ustawi bora katika jamii.
Rhobi ameongeza kuwa, wadau mbalimbali wanawajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali na Chama Cha Mapinduzi kusukuma mbele gurudumu la maendeleo bila kurudi nyuma hasa kuyawezesha makundi maalum na watu wasiojiweza kupata mahitaji ya msingi sambamba na kushirikiana nao kwa karibu.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa CATA MINING, John John amesema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa makundi yenye uhitaji katika jamii hawakusita kutoa msaada huo baada ya kupokea barua ya kuombwa kusaidia na UWT Mkoa wa Mara kwani ni njia mojawapo wa kuimarisha ustawi bora na uhusiano katika jamii.