CCM yaonya wataalamu, madiwani wenye tabia za kutoka nje wakati vikao vikiendelea wilayani Simanjiro

NA MARY MARGWE

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Amos Shimba amewataka wataalamu wa halmashauri pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanaacha kabisa tabia ya kutoka toka wakati vikao vikiwa vinaendelea.
Hayo ameyabainisha alipokuwa kwenye kikao cha baraza hilo, ambapo alisema kikiwa ni kikao chake cha kwanza cha baraza kuhudhuria ameona mengi na ameona ni vema kuwekana sawa ili kulinda heshima ya kikao hicho.

Shimba amesema, ni kitendo cha aibu kuona madiwani wanatoka toka nje huku wataalam nao hali kadhalika huku wakijuea kabisa kuwa hicho ni kikao muhimu na cha kisheria, hivyo ni vema wakakipa heshima yake.
"Kama ambavyo nilisema awali mimi naendelea kujifunza, naona wataalam na madiwani pia nao wanatoka toka sana ukumbini huku kikao kikiendelea, jamani ni aibu narudia ni aibu sana hivi ukiona viti viko wazi ni dharura wote? Alihoji Katibu Shimba.

Aidha,alisema kikao hicho ni cha kujenga hivyo kinachotakiwa ni kukaa kwa utulivu, kusikiliza na kujenga hoja ya msingi ili kuweza kuchangia kama kuna uhitaji huo, na sio kutoka toka nje kila wakati, kunasababisha kushusha heshima ya kikao na kufanya mwendesha kikao akose nguvu ya kuendelea na kikao.

Aidha, alitolea mfano kwa wataalam waliokuwa wakitoka toka nje, kwani kunaweza kutokea diwani akauliza swali kwenye kuhusika na kujibu ni mtaalam ambaye ametoka nje, ndipo Mkurugenzi atatakiwa kujibu badala yake.

"Hiki ni kikao cha kisheria sisi kama Chama Tawala yaani CCM tukipata nafasi tunakuwa tunaongea nanyi yaani madiwani na wataalam kupitia kikao hiki juu ya mambo mbalimbali ya kuwekana sawa ili kuijenga serikali yetu, kwani hapa ni mahala pa kushirikiana bainan yetu , wataalam na madiwani ili kusukuma gurudumu la maendeleo mbele," alifafanua Katibu huyo wa CCM.
Pia alimtaka Mkurugenzi kuhakikisha anawaambia watendaji wa Kata kuweza kuwaandalia taarifa nzuri madiwani ikiwa ni pamoja na kuwapatia siku kadhaa kabla ya baraza ili kumuwesha diwani kuipitia na iwapo kuna sehemu ina uhitaji wa kuirekebisha basi aweze kurekebisha, badala ya kuwapatia siku ya kikao.

"Uandaaji wa taarifa, nimeona baadhi ya watendaji wa kata wakiwapatia waheshimiwa madiwani taarifa muda huu wakati wengine wakiendelea kuwasilisha taarifa zao, sasa haya mapungufu yasijirudie tena, diwani atakuwa ameipitia taarifa hiyo muda gani na kurekebisha muda gani, Mkurugenzi fuatilia hili ili taarifa ziweze kuandaliwa vizuri na kwa ufasaha kwa waheshimiwa madiwani, taarifa ya miezi mitatu mheshimiwa diwani analetewa leo ukumbini haipendezi kabisa," alisema Shimba.
Aidha, pia alimtaka Mkurugenzi kuhakikisha anapeleka walimu wa kike katika shule zisizo na walimu wa kike ili kuweza kuwasaidia watoto wa kike watakapohitaji kupata huduma kwa mwalimu wa kike, hilo lizingatiwe na lifanyike kazi haraka maana madiwani wameliongelea sana jambo hilo.
Hata hivyo ameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanawawekea vibao vitakavyowatambulisha madiwani kwa jina na Kata ama tarafa yake kwa wale madiwani wa viti maalum, huku pia akiongeza kuhakikisha halmashauri inaweka vipaza sauti ukumbini ili kuwarahisishia madiwani kusikika kwa urahisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news