China yagusa maisha ya wananchi Zanzibar kupitia Wakfu wa Maisha Bora

NA MWANDISHI DIRAMAKINI 

BALOZI wa China nchini Tanzania, Zhang Zhisheng amesema msaada wa vyerahani uliotolewa na Ubalozi huo kwa Jumuiya ya 'Zanzibar Maisha Bora Foundation' unalenga kuwawezesha wanawake wa Zanzibar ili kuondokana na umaskini.

Balozi Zhang amesema hayo wakati alipokabidhi vyerahani nane kwa Uongozi wa Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, hafla iliofanyika katika Ubalozi huo,uliopo Mazizini jijini Zanzibar. 

Amesema, msaada wa vyerahani hivyo vinane, ni mwanzo wa misaada mbalimbali inayolengwa kutolewa na Ubalozi huo kwa jumuiya hiyo ili kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kuinua maisha yao.
Naye Mtendaji Mkuu wa jumuiya hiyo, Mwanaidi Mohamed Ali kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mama Mariam Mwinyi aliushukuru Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa msaada huo, na kusema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Ubalozi huo katika kushirikiana na jumuiya hiyo ili kuwawezesha wanawake Zanzibar.

Pia amesema, Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation inathamini msaada huo na itaendelea kushirikiana na Ubalozi huo, huku akiahidi kutumika vyema kwa malengo yaliokusudia. 

Msaada wa vyerahani vinane uliotolewa na Ubalozi wa China nchini Tanzania, unatokana na mkutano wa wadau uliofanyika Januari 26, mwaka huu katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar –Airport, uliolenga kuwahamaisha wadau mbalimbali kushirikiana na jumuiya hiyo ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa. 

Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation,ambapo malengo yake makuu ni kuinua maisha ya wanawake wa Zanzibar kuondokana na umasikini,inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi ujao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news