DC Msafiri abisha hodi kiwanda bubu cha kuzalisha mafuta ya mawese, atoa tamko

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Sara Msafiri amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kuvifungia viwanda kinyume na utaratibu na badala yake waziachie mamlaka udhibiti ubora zinazohusika na masuala hayo zifanye kazi yake.
Amesema,kazi ya jeshi hilo ni kushughulika na masuala ya jinai na kama kuna masuala ya mtambuka mtu kufanya uzalishaji ni vyema wanaohusika wakaachiwa wafanye kazi yao.

Msafiri ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea kiwanda bubu cha kuzalisha mafuta ya Mawese kilichopo Kongowe Kibaha kinachomilikiwa na Halifa Issa ambacho kilifungwa na Jeshi na Polisi na kuchukua madumu ya mafuta 40 na baadhi ya vifaa vya kiwanda hicho.

Baada ya Jeshi la Polisi kukifunga kiwanda hicho taarifa zilifika kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na hivyo kumuagiza Mkuu huyo wa Wilaya kwenda kiwandani hapo kwa ajili ya kumsaidia mjasiriamali huyo.

Akiwa kiwandani hapo, Msafiri amesema Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kukifungia kiwanda chochote kwa kuwa wanaohusika na masuala ya udhibiti ubora wa bidhaa wapo na wapo wanachotakiwa kufanya ni kushughulikia jinai.
"Mtu anafanya uzalishaji,amejiajiri,na anajipatia kipato,kwa hiyo hatujafikia hatua ya kuhoji ubora wa bidhaa yake kwani zipo mamlaka za kuhoji,sisi tushughulike na jinai,"amesema Msafiri.

Msafiri,amesema kuwa kama kuna mapungufu yoyote katika kiwanda wazijulishe mamlaka za udhibiti ubora ambazo ndizo zinatakiwa kusajili viwanda,kutoa vitambulisho,na masuala mengine yote.

"Watu wa mazingira wapo ndio kazi yao kuja na kama wataridhika na uzalishaji au wataona mapungufu basi wawasaidie ili watekeleze hizo Standard ( viwango vinavyotakiwa) ili waweze kuendelea kuzalisha,"amesema Msafiri.

Msafiri,ameongeza kuwa wakisema kila wanapoenda wafungie viwanda tafsiri yake ni kuwa itatokea siku mtu wa Dawasa ataenda kwenye kiwanda kinachozalisha bidhaa zenye ubora ,kilichoajiri watu ,kinalipa Kodi na huduma nyingine wanalipwa lakini kwasababu hajalipa Dawasa basi kiwanda kifungwe.

Amesema kuwa,wakiruhusu kila mtu akachukua cha kwake ambacho hakijafanyika katika kile kiwanda basi viwanda vyote vitafungwa na uzalishaji utashuka.

"Sasa Jeshi la Polisi mimi sitaki kuhusika na kesi ya jinai ,kama kuna jinai yoyote iendelee na chunguzeni lakini masuala yote ya mamlaka zote za udhibiti ubora wakiwemo wa mazingira waende hapo kiwandani wawashauri vijana wafanyeje ili wakidhi viwango,"amesema.

Aidha,amelitaka Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) wafike kiwandani hapo ili waone namna ya kuwasaidia vijana wajasiriamali wa kiwanda hicho na kwamba inapaswa kuwajengea uwezo. 

"Mamlaka ya udhibiti ubora tunatakiwa kuwasaidia vijana hao kwa kuwajengea uwezo ili wakuze mitaji yao na wafanyekazi katika mazingira salama na tunatakiwa kuwasaidia kwakuwa wameamua kujiajiri ,"ameongeza Msafiri.
Hata hivyo,mmiliki wa kiwanda hicho Halifa Issa (42) Mkazi wa Kongowe Kibaha alikamatwa na Jeshi la Polisi juzi kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya Mawese bila kufuata utaratibu na hivyo kuchukuliwa vifaa vyake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news