NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MKUU wa Wilaya ya Njombe mkoani Njombe, Kissa Gwakisa amefika katika Shule ya Sekondari Mpechi iliyopo katika Halmashauri ya Mji Njombe na kuangalia zoezi la kuripoti kidato cha kwanza katika shule hiyo.
Akitoa taarifa fupi ya tathmini ya hali ya kuripoti kwa Wanafunzi wa Kidato cha kwanza Shuleni kwa kipindi cha siku mbili tangu kufunguliwa kwa shule mnamo tarehe 17/01/2022, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mpechi, Brown Kiswaga amesema kuwa mpaka kufikia tarehe 18/1/2022 takribani nusu ya wanafunzi waliopangiwa shuleni hapo wamesharipoti na wameanza masomo na amewahimiza wazazi kuendelea kuwapeleka watoto shuleni kuripoti.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe ameoneshwa kuridhishwa na hali ya Wanafunzi kuripoti shuleni hapo na ameipongeza Shule hiyo kwa kuendelea kuimarisha kiwango cha taaluma shuleni hapo na kuwapongeza kwa kuendelea kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya pia ametembelea na kujionea hali halisi ya matumizi ya madarasa mapya yaliyojengwa na Serikali kupitia mpango wa Taifa wa kupambana na UVIKO ambapo akiwa Shuleni hapo ameweza kujione Wananfunzi wa Kidato cha kwanza wakiwa katika vyumba vipya vya madarasa na wakifurahia mazingira mazuri ya kujifunzia na kujisomea.