NA SOPHIA FUNDI
WATUMISHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha pamoja na baadhi ya wananchi leo wamejitokeza kufanya usafi katika maeneo ya hospitali mpya ya wilaya ikiwa ni siku ya Maadimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Karia Magaro amesema kuwa, katika kuadhimisha siku ya Mapinduzi watumishi walikubaliana kufanya usafi katika hospitali hiyo mpya ya wilaya ambayo ujenzi wake unaendelea.
Picha ikiwaonyesha mkuu wa wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba aliyevaa kofia na mkurugenzi wa halmashauri, Karia Magaro mwenye tisheti nyeupe wakiongoza zoezi la usafi katika hospitali mpya ya wilaya.
Magaro amesema kuwa, zoezi la kufanya usafi katika mazingira ya hospitali litakuwa endelevu ambapo amewaomba wananchi pale watakaposikia matangazo ya usafi katika eneo hilo wajitokeze kwa wingi ili kuyafanya mazingira ya hospitali yawe mazingira yanayofaa kwa huduma pale itakapofunguliwa.
John Lucian ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa upande wake amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ambayo itakuwa ya historia kwa wananchi wa Karatu, kwani wilaya hiyo haikuwa na hospitali ya wilaya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba amewashukuru watumishi pamoja na wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo la maadimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kufanya usafi katika mazingira ya hospitali ya wilaya.
"Leo ni siku ya mapumziko, lakini mmekuja kufanya usafi hapa hospitali, serikali ya wilaya tunawashukuru sana na zoezi hili liwe endelevu kwa wilaya yetu,"amesema Kolimba.