Diwani Salome Mnyawi aiomba Serikali Kituo cha Afya

NA MARY MARGWE

DIWANI wa Kata ya Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Salome Mnyawi ameiomba serikali kuwajengea kituo cha afya, kwani kata hiyo haina kituo cha afya wala zahanati ya serikali, zilizopo ni zahanati mbili za watu binafsi ambazo gharama zao ziko juu ukilinganisha na vituo vya serikali.
Hayo ameyabainisha alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya Kata ya Mirerani kwa kipindi cha miezi mitatu (Oktoba - Desemba 2021) kwenye baraza la madiwani la halmashauri hiyo, lililoketi chini ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Sendeu Laizer.

Mnyawi amesema, wananchi wa Kata ya Mirerani wanapata huduma za matibabu kupitia zahanati mbili za watu binafsi ambazo ni Mico (kwa Minja ) na Moipo Dispensary ambazo zote zinatoa huduma kwa wananchi lakini kwa gharama kubwa sana, hivyo ameiomba iwajengee wananchi wa Kata ya Mirerani kituo cha afya. 

"Mheshimiwa mwenyekiti mimi ndiye mwakilishi wa wananchi wa Kata ya Mirerani naomba nilete ombi la Kata ya Mirerani kujengewa kituo cha afya, kwani hatuna kituo cha afya wala zahanati ya serikali, zahanati mbili zilizopo ni za watu binafsi ambazo wananchi wamekuwa wakinilalamikia kuwa gharama zao ziko juu sana, hivyo tunaomba serikali ituangalie kwa uhitaji huo mkubwa wa huduma za afya Mirerani," alisema Salome Mnyawi.

Alisema, wananchi wa Kata ya Mirerani sasa ni wakati wao wa kupatiwa kituo cha afya ili waweze kupata huduma za afya kama ambavyo sehemu nyingine wanapata.

Aidha, alisema kwa kuwa serikali ya chama cha mapinduzi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na yenye kuwajali wanyonge ana imani itakua imesikia na anaamini itatekeleza ombi hilo haraka iwezekanavyo ili kuendelea kulinda imani yao kwa ccm na hatimaye kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika tukio lingine Kata hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya barabara kutokupitika kutokana na uharibifu maji ya mvua ambapo yamekata mawasiliano kati ya mtaa na mtaa, hivyo ameiomba TARURA kwenda kuangalia na kutengeneza barabara zote za vitongoji hususani kitongoji cha Kwanyiti ambako barabarazake nyingi zimeharibiwa sana na mvua.

"Pia barabara ya kutoka geti la Magufuli hadi shule ya sekondari Tanzanite imeharibika kabisa, hivyo ni vema TARURA ikaja kwenda kuangalia na kutengeneza barabara zote za vitongoji hususani kitongoji cha Kwanyiti ambako barabarazake nyingi zimeharibiwa sana na mvua," alisema Diwani wa Kata hiyo ya Mirerani.

Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wananchi, pamoja na wadau mbalimbali lakini bado Kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa kwa shule zote za msingi na sekondari kutokana na idadi ya wanafunzi katika shule hizo.

Changamoto nyingine ni upatikanaji wa huduma ya maji katika shule ya sekondari Tanzanite, hivyo ameiomba RUWASA kuwakumbuka wakati wa utengenezaji wa mradi wa Maji Mirerani, pia katika shule ya msingi Songambele wana ukosefu wa darasa rafiki kwa wanafunzi kwenye uhitaji maalum.

Hata hivyo pia Diwani Mnyawi ameiomba halmashauri hiyo iwasaidie kukarabati madarasa chakavu katika shule ya msingi songambele, pia halmashauri iwasaidie namna ya kukabiliana na upungufu wa nyumbani za walimu katika shule za msingi na sekondari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news