NA TITO MSELLEM-WM
IMEELEZWA kuwa, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na viongozi wa Serikali wana wajibu wa kutoa elimu juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 2022 ili wananchi waweze kutoa ushirikiano pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kufanikisha lengo la zoezi hilo.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote waliopo ndani ya nchi kwa umri, jinsia,mahali wanapoishi, hali ya elimu, ajira, vizazi, vifo na makazi ambapo misingi hiyo ndiyo inayoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi yenye uhitaji maalum kama vile watu wenye ulemavu, watoto, wanawake, vijana na wazee.
“Natambua viongozi wa Dini zote na viongozi wa Kimila wana jukumu kubwa la kuwa viungo kati ya serikali na wananchi na ili kudumisha amani kupitia nyumba za ibada kwa kufundisha maadili mema kama vitabu vitakatifu vinavyoelekeza na Nina imani viongozi wote mliokuja Leo mnauwezi wa kuelimisha jamii kutokana na nyazifa zenu,”amesema Dkt.Kiruswa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha Leokadia Mtey amesema kuwa Sensa itaisaidia serikali kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo kwani inategemea takwimu katika kufanya shughuli za maendeleo ya nchi ambapo sensa hiyo itakuwa ni sensa ya 6 tangu nchi kupata Uhuru mwaka 1961.
Athanas amesema kuwa, watu wanaostahili kuhesabiwa ni watu wote waliolala ndani ya mipaka ya Tanzania ambapo lengo kuu ni kuhakikisha kwamba kila mtu aliyelala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa anahesabiwa na atahesabiwa mara moja.
“Sensa inayoenda kufanyika ipo kiutaratibu na miongozo na taarifa zote binafsi za watu zitakazokusanywa ni siri na zitatumika kwa madhumuni ya takwimu tuu hivyo wananchi msiogope kutoa taarifa sahihi kwani wakitoa taarifa za uongo itafanya serikali ipange mipango ambayo haitakiwa na manufaa kwa wananchi,” amesema Mtey.
Pia, Mleya amesema kuwa, Serikali wakati inapanga mipango yake, bila kuwa na taarifa sahihi haiwawezi kujua wapi panahitaji jambo fulani au wapi kuna changamoto zinazohitajika kutatuliwa ili wananchi waweze kufikiwa na huduma za kimaendeleo hususan huduma za kijamii ambapo kwa mara ya kwanza sensa ya watu na makazi itafanyika kwa kwa kutumia vifaa vya kisasa kama vishkwambi (tablet) tofauti na awali ambapo ilikuwa ikifanyika kwa kutumia makaratasi.
Naye Katibu wa Taasisi ya Twariqa Tanzania Yahaya Athman Mkindi amesema kuwa zoezi hili ni muhimu kwa kuwa litawasaidia serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta ya mbali mbali kama elimu,afya,hali ya ajira,miundombinu ya barabara nishati na maji safi.