Dkt.Tulia Ackson Spika wa saba Bunge la Tanzania?

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson anatarajiwa kuvaa viatu vya aliyekuwa Spika wa Bunge hilo ambaye alijiuzulu hivi karibuni, Mheshimiwa Job Ndugai.
Hayo yanajiri baada ya leo Januari 20,2022 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitisha jina la Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kamati hiyo imeketi leo jijini Dodoma ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Iwapo, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson atashinda nafasi hiyo atakuwa Spika wa saba tangu Uhuru akiwa ametanguliwa na Chifu Adam Sapi Mkwawa, Chifu Erasto Mang'enya, Pius Msekwa, Samuel Sitta, Anne Makinda na Job Ndugai.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 84,inataja sifa zifuatazo kuwa Spika; "(1) Kutakuwa na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au wenye sifa za kuwa wabunge; atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge".

Hii maana yake ni kuwa Spika anaweza kutoka miongoni mwa wabunge na wasio wabunge ili mradi anatimiza sifa za kikatiba. 

Aidha, kupata sifa za mtu anayeweza kuwa mbunge pamoja na mambo mengine, Katiba inataja sifa kama vile kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria, kuwa na umri wa zaidi ya miaka 21, kutokuwa waziri au naibu waziri, kuwa na akili timamu na kutowahi kuhusishwa na makosa ya uhaini.

Uteuzi wa Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson unaitimisha maombi ya watu zaidi 70 ambao walijitokeza katika chama hicho kuomba ridhaa ya kuwania nafasi hiyo.

Katika historia ya Bunge la Tanzania, kumekuwa na sifa kadhaa zisizo katika Katiba wala sheria zozote, ambazo ziliwapa maspika waliotangulia fursa ya kupata nafasi hiyo adhimu na hivyo kuongoza chombo hicho ambacho kazi zake kuu ni kutunga sheria na kuisimamia serikali.

Chifu Mkwawa na mwenzake Chifu Abdieli Shangali, walikuwa Watanganyika weusi wa kwanza kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria mnamo mwaka 1947. 

Wakati Tanganyika inapata Uhuru wake mwaka 1961, Mkwawa tayari alikuwa mbunge kwa takribani miaka 14. Ndiye alikuwa mbunge wa muda mrefu zaidi kupita wengine.

Msekwa alikuwa bungeni kabla ya Uhuru akiwa Naibu Katibu wa Bunge na baadaye kuja kuwa Mbunge wa Ukerewe na wakati anachaguliwa kuwa Spika, tayari alikuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 ndani ya mhimili huo.

Aidha,Mheshimiwa Makinda na Hayati Sitta nao walikuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 30 kama wabunge kabla ya kuchaguliwa kuwa spika wa Bunge. 

Kwa sababu hiyo, hata kama haijaandikwa popote kwenye sheria, kuwa mbunge mzoefu kuna sifa ya ziada kwa yeyote anayewania nafasi hiyo.

Naibu Spika

Pia historia ya Bunge la Tanzania inatuonyesha pia kwamba katika maspika sita waliotangulia, watatu kati yao walikuwa kwanza manaibu spika kabla ya kuwa maspika. 

Maspika hao ni Msekwa, Makinda na Ndugai. Hii maana yake ni kwamba kimahesabu, ukiwa Naibu Spika una nafasi kubwa ya kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news