NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MBUNGE wa Geita Vijijini (CCM),Dkt. Joseph Kasheku (Msukuma) amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msukuma amechukua fomu hiyo leo Jumanne Januari 11, 2022 katika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni, Mheshimiwa Msukuma ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima ya Siasa na Uongozi kutoka chuo cha The American University.
Msukuma na wenzake 15 akiwemo mwanaharakati Flora Lauo wa Nitetee Foundation na aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo ambaye ni Mbunge wa Vwawa mkoani Songwa, Japhet Hasunga nao walitunukiwa.
Shahada hizo walitunukiwa mkoani Dodoma na Profesa Madhu Krishan, mwakilishi wa chuo hicho.
Kuhusu Elimu
Msukuma mwenye elimu ya darasa la saba alisema chuo hicho kwa kipindi cha miaka mitatu kilikuwa kinafuatilia michango yake bungeni kupitia video za YOUTUBE na alikuwa akipigiwa simu mara kwa mara kwa ajili ya kumfuatilia mpaka Desemba 5,2021 ambapo alitunukiwa heshima hiyo.