NA FREDY MGUNDA
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Hassan Moyo ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto ya vyumba vya madarasa ambayo yatasaidia wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kupata nafasi katika mwaka huu wa masomo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga akikagua vyumba vya madarasa akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Iringa,Mohamed Hassan Moyo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa, Stephen Mhapa mara baada ya kukabidhiwa vyumba ambavyo vimekamili kwa asilimia 100.
Amezungumza hayo wakati wa kukabidhi vyumba vya madarasa 94 kwa mkuu wa mkoa wa Iringa ambavyo vimejengwa kupitia mradi wa 5441 TCRP ambavyo vyumba vya madarasa ya sekondari ni 66 na shule shikizi 28 katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Moyo amesema kuwa, anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan kwa namna ambavyo amefanikiwa kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19 na kufanikiwa kupata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) wa kiasi cha shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kusaidia kufufua uchumi katika sekta ambazo zimeathirika kutokana na janga hilo.
Amesema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ilipokea kiasi zaidi ya shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari 66,shule shikizi 28 na nyumba za walimu kwa ajili ya maendeleo ya kukuza sekta ya elimu pamoja na ujenzi wa wodi katika sekta ya afya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bashir Mhoja akiwaonyesha ubora wa vyumba vya madarasa Mkuu wa mkoa wa Iringa, Queen Sendiga na mkuu wa wilaya ya Iringa, Mohamed Hassan Moyo.Moyo alisema kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo ulianza mwanzoni mwa mwezi wa kumi na moja mwaka 2021 na kukamilika kabla ya tarehe saba mwezi wa kwanza mwaka 2022.
Alisema kuwa, ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa umekuja kutokana na idadi ya wanafunzi ambao watajiunga kuanzia mwenzi wa kwanza mwaka huu 2022 ambapo inajumuisha viti na madawati.
Aidha moyo alisema kuwa hakuna mwanafunzi atakayekosa sehemu ya kukaa akiwa amechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule yeyote ilivyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa na kuwahimiza wazazi kuwapeleka shule wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza.
Moyo aliongeza kuwa lengo la kujenga vyumba vya madarasa 28 vya shule shikizi ni kuwapunguzia adha wanafunzi wanaotoka mbali na maeneo ambayo shule mama ipo ili nao waweze kupata elimu iliyo bora kama wanafunzi wengine.
Moyo alimalizia kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha hizo ambazo zimesaidia kutatua changamoto hiyo ambavyo ilikuwa inawakabiri wananchi na kuongeza ajira za muda kwa wale waliokuwa wanafanya kazi ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa hayo.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga alisema ujenzi wa vyumba vya madarasa 94 sio jambo rahisi kwa Halmashauri hivyo ameupongeza uongozi wa halmashuri hiyo kwa kazi kubwa ya kusimamia ujenzi huo kukamilika kwa wakati.
“Alinipigia simu baba yangu na kuniuliza kuwa wewe mtoto wangu kwenye mkoa wako unajenga madarasa mangapi? Nikamjibu kuwa nina madarasa akasema kuwa huyo binti yangu Samia kazi aliyoifanya haijawahi kufanywa na kiongozi yeyote Yule toka apate akiri na ilikuwa inachukua miaka mnne kupata darasa moja ili watoto waweze kusoma ndio maana watoto wengi walikuwa wanashindwa kuendelea na masomo,” alisema RC Sendiga.
Sendiga alisema kuwa jitihada hizo ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambayo hayajawahi kufanywa na kiongozi mkubwa kaka yeye ndio maana ameweka historia ya kipekee.
Alisema kuwa, miaka ya nyuma ilikuwa ikifika kipindi kama hiki wazazi wengi hukimbia makazi yao kutokana na kukimbia majukumu ya kuchangia ujenzi wa madarasa na elimu ya watoto wao na wazazi wengine hulazimika kuuza mali zao ili kumudu kugharamia elimu ya watoto.
Sendiga alisema kuwa watanzania wanatakiwa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake anazozifanya za kuleta maendeleo ya nchi.
Aidha, Sendiga alisema kuwa miradi yote aliyoitembelea siku ya leo imekuwa miradi bora na yenye viwango ambavyo vinatakiwa hivyo aliwapongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa kwa kusimamia vilivyo miradi hiyo ya kimaendeleo.
Aliwataka wazazi kuwapeleka shule watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwa serikani tayari imepokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum hivyo wazazi hawapaswi kabisa kuwafungia watoto hao badala yake wanatakiwa kuwapeleka shule.
Alisema katika miradi ya maji ambayo ameikagua kwa kiasi kikubwa imemlizisha kwa namna ambavyo imetekelezwa na kuhakikisha inamtua ndoo mwanamke kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anayotaka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Stephen Mhapa alisema kuwa watumishi wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kila mradi unatekelezwa kwenye Halmashauri hiyo unatekelezwa kwa wakati na ubora unatakiwa kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya mradi.
Mhapa alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakiwakatisha tamaa watumishi hao kwa kuongea maneno magumu tofauti na uhalisia wa kazi ambazo wanazitekeleza.