NA MWANDISHI MAALUM
HIFADHI ya Taifa Serengeti imeboresha shughuli za utalii na kuongeza uzoefu kwa watalii wanaotembelea hifadhi kwa kujenga vibao maalumu 'interpretative panels' vya maelezo kwa vivutio vya kiutamaduni vilivyopo ndani ya eneo la Moru.
Hayo yamebainishwa leo Januari 16, 2022 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi -Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete.
"Sambamba na watalii kupata fursa ya kipekee ya kuona Faru weusi ndani ya eneo la Moru pekee, watalii watapata maelezo ya vivuvito vya kitamaduni vya kipekee kupitia vibao hivyo ikiwemo maisha ya kabila la Dorobo na Masai namna walivyoishi na wanyamapori, matambiko yao na wanyama walioheshimika zaidi na kwanini.Karibu Serengeti kwa uzoefu wa kipekee ndani ya Eneo la Moru,"amefafanua Kamshina Shelutete.
Ameongeza kuwa, utafurahia kuona Faru weusi, historia na tamaduni za watu wa kale ikiwemo Masai rock paints , Gong rocks na historia ya wanyama hao adimu Faru weusi.
Kuhusu Hifadhi ya Taifa Serengeti
Kwa mujibu wa Tovuti Kuu ya Serikali, hii ni hifadhi kongwe zaidi na maarufu, pia ni eneo la urithi duniani, na hivi karibuni imetangazwa kuwa maajabu saba ya dunia, ipo umbali wa kilomita 335 (sawa na maili 208) kutoka Arusha, imeenea Kaskazini hadi Kenya na kupatikana na Ziwa Victoria upande wa Magharibi. Ina ukubwa wa kilomita za mraba 14,763 (sawa na maili za mraba 5,700).
Serengeti ni maarufu kwa uhamaji wa wanyama wa kila mwaka wakiwemo nyumbu ambapo wanyama wenye kwato milioni sita wanakanyaga uwanda wa wazi, wakati zaidi ya pundamilia 200,000 na swala wa Thomson 300,000 wanajiunga na safari ndefu na ngumu ya nyumbu kutafuta malisho mapya.
Hata kama uhamaji huo umetulia, hakuna ubishi kwamba Serengeti ina mandhari ya kuvutia ya kuangalia wanyama barani Afrika: makundi makubwa ya nyati, vikundi vidogo vya tembo na twiga na maelfu kwa maelfu ya pofu, topi, kongoni, swalapala, na swala wa Grant.
Kuhimili kama ilivyo utazamaji wanyama ni hisia ya ukombozi wa nafasi ambayo ni sifa bainifu ya Uwanda wa Sengereti, unaoenea kwenye savana inayopigwa na jua hadi katika upeo wa dhahabu unaometameta jua linapokuchwa.
Hata hivyo, baada ya mvua kunyesha, eneo hili kubwa la rangi ya dhahabu, linageuzwa kuwa zulia la kijani lililonakshiwa mauapori. Aidha kuna milima yenye miti na vichuguu vya mchwa vilivyochomoza, mito ikiwa na kingo zenye miti ya mitini na mapori ya mijohoro yenye rangi ya njano kutokana na vumbi.
Bila ya kujali umaarufu wa Serengeti, bado inabaki kuwa hifadhi kubwa ambapo unaweza kuwa binadamu pekee kuona, wakati samba anapofikiria kuzingira kwa fahari, bila ya kutetereka kwenye mlo wake unaofuata.Kwa taarifa zaidi fungua tovuti yetu: http://www.serengeti.org
Jinsi ya Kufika Serengeti
Kupanda ndege za kawaida na za kukodi kutoka Arusha, Ziwa Manyara na Mwanza. Kusafiri kwa gari kutoka Arusha, Ziwa Manyara, Tarangire au Ngorongoro Kreta.