NA MWANDISHI MAALUM- WAF
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa Morogoro, imeimarisha huduma ndani ya wodi ya kujifungua wazazi pamoja na hali ya upatikanaji wa dawa.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi, alipofanya ziara kwa lengo la kukagua huduma za tiba zinazotolewa hospitalini hapo.
"Zamani dawa zilikua kwa kiwango cha chini sana, wagonjwa walikua wakienda nje kununua lakini kwa sasa zinapatikana ndani na tatizo hilo limepungua japo halijakwisha kabisa kwa kuwa imeongezeka asilimia 70-85,"amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi amewataka wauguzi na waganga wa hospitali hiyo kufanya juhudi zaidi ili kuweza kuzifikia asilimia 15 zilizosalia, wagonjwa wote wapate dawa ndani ya hospitali.
"Swala la vipimo vingi vimekuwa vikipatikana japo kuna changamoto chache ambazo tunahitaji kuziboresha kwa kuhakikisha vipimo vyote vya msingi vinapatikana hapa,"amesema.
Pamoja na hilo, ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuisaidia hospitali hiyo ili kuhakikisha inaweza kufanya vipimo vyote vinavyotakiwa kwa mashine.
Prof. Makubi amebainisha wizara ya Afya imeshaweka fedha katika hospitali hiyo kwa ajili ya ujenzi wa miradi elekezi ya wodi mbalimbali ambapo uongozi umeahidi watatumia muda wa miezi minne kukamilisha.
Katika kikao chake na viongozi wa hospitali hiy, Prof. Makubi amewataka kuhakikisha wanafanya kazi kwa uaminifu na weledi mkubwa ili kuwahudumia vizuri wagonjwa.
Amewataka kusimamia vizuri fedha za Serikali kwa kufanya miradi elekezi kwa kuwa fedha hizo hutolewa kwa malengo.
"Nawaagiza muendelee kutafuta vyanzo vya fedha ili majengo ambayo tayari mmeshaanza kuyajenga myamalize kama lile la upasuaji ili Madaktari wa upasuaji waweze kutoa huduma zao,"amesema Prof. Makubi.
Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Mganga Mkuu Mkoa-Morogoro Dkt. Kusirye Ukio na Mkurugenzi msaidizi anayesimamia Hospitali za Mikoa, idara ya Tiba, Wizara ya AFYA Dkt. Caroline Damian Mayengo.