PRISCA ULOMI NA DAUDI MANONGI
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA yenye urefu wa kilomita 265 ambao umefanyika kwenye eneo la Itigi, Manyoni mkoani Singida hadi eneo la Kambikatoto, Mbeya.
Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 265, vituo vya kutolea huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vituo vya kuongeza nguvu za mawasiliano.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akikagua kituo cha maunganisho ya Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Manyoni, Singida mpaka Kambikatoto mkoani Mbeya.
Dkt. Yonazi amesema kuwa amefanya ziara hiyo ili kukagua ujenzi huo kwa lengo la kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo ili kuona namna mkandarasi ametekeleza kazi husika kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni nane za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo iliyojengwa eneo la Itigi, Manyoni hadi Kambikatoto
Ameongeza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano, za uhakika na kwa gharama nafuu katika maeneo yote nchini nzima ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanaendelea kutumika katika shughuli za kiuchumi na kijamii katika kuchochea maendeleo ya taifa letu.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akisoma kipimo kinachoonesha urefu na ubora wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa akiwa kwenye kituo cha kutolea huduma za Mkongo cha Rungwa wakati ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Manyoni, Singida mpaka Kambikatoto mkoani Mbeya.
Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Rajab Mikumwo wa Kampuni ya Raddy Fibre Solutions ambaye ni mkandarasi aliyejenga miundombinu hiyo amemweleza Dkt. Yonazi kuwa, kampuni yao imetekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo kwa mujibu wa matakwa ya mkataba na tayari nyaya za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zimelazwa ardhini na katika baadhi ya maeneo nyaya hizo zimepitishwa juu ya nguzo kuendana na jiografia ya eneo husika endapo kuna mto au mwamba ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanapatikana kwa uhakika mwanzo hadi mwisho wa eneo husika.
Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mulembwa Munaku akielezea jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi wakati Katibu Mkuu huyo alipofanya ziara kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Manyoni, Singida mpaka Kambikatoto mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa tayari Serikali imefikisha miundombinu hiyo kwenye maeneo ya mipaka ya nchi za jirani zinazopakana na Tanzania na sasa hatua zinaendelea za kufikisha mawasiliano hayo mpakani mwa DRC Congo na Tanzania ili nchi jirani ziendelee kutumia na kunufaika na miundombinu hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Nikusubila Maiko akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonaz juu ya ubora wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu huyo ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Mnyon, Singidai mpaka Kambikatoto, Mbeya.
Mhandisi wa kuunganisha waya wa Mkongo, Evanda Luvanda wa Kampuni ya Raddy Fibre Solution, akieleza urefu na ubora wa mkongo huo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi wakati wa ziara ya Katibu Mkuu huyo kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Mnyoni, Singida mpaka kambikatoto, Mbeya.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mhandisi Nikusubila Maiko amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utawezesha watoa huduma za mawasiliano nchini kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kuwa tayari watoa huduma hao wamewasilisha mahitaji hayo Wizarani ambapo ujenzi wa miundombinu hiyo utaongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi walio kwenye maeneo hayo ambapo miundombinu hiyo imejengwa.