Anaandika Msemaji Mkuu wa Serikali, ndugu Gerson Msigwa....
Jana baada ya kutoka Njombe nilikotoa Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali, nilikwenda kumuona huyu Bibi anayeishi kando ya Shule ya Sekondari Mtwango. Jina lake ni Edina Nyawumbu.
Nikiwa nasoma Shule ya Sekondari Mtwango, huyu Bibi alikuwa na mgahawa nyumbani kwake anauza chai na chakula.
Nilipokuwa na visenti nilikwenda ku change diet (sh. 100 unapata chai na maandazi mawili), pesa yangu ya matumizi ilikuwa haizidi shilingi 500 kwa miezi mitatu.
Kwa hiyo niliishiwa kwa muda mfupi na baada ya kuishiwa sikuwa nakwenda mgahawani kwake.
Alipogundua alikuwa anawatuma wenzangu waniite nikanywe chai, nikifika namwambia sina hela anasema wewe kunywa tu. Nilikunywa mara nyingi, sikuwa na pesa ya kulipa na hakuwahi kunidai.
Siku nilipomaliza shule alikuja kwenye mahafari akawa kama mzazi wangu kwa sababu sikuwa na ndugu waliokuja, alinivalisha taji, akanipigia vigelegele na akaniombea maisha marefu na mafanikio.
Baada ya hapo sikuwahi kuonana nae hadi jana nilipomtembelea kwa surprise, ikalazimu nijitambulishe kwa sababu alishanisahau.
Kwa miaka yote nimekuwa nikimkumbuka sana huyu Bibi na kutafakari wema wake usio na kipimo kwa watoto wa Wanawake wenzie. Nyuma ya hizo picha ni Sekondari ya Mtwango.
Somo
1. Wema hauozi.
2. Tusiwasahau walionyuma ya uhai wetu na mahali tulipo.
3. Tuwapende na kuwasapoti watoto wanaopigania ndoto zao.